MAFURIKO YAKOSESHA MAKAZI KAYA 235 KYELA

Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe amesema kaya 235 zenye wakazi 1,087 katika wilaya hiyo, zipo katika hali mbaya.
Amesema kaya hizo zimeathiriwa vibaya na mafuriko, yaliyoikumba wilaya hiyo na kwamba sasa zimehamishiwa kwenye makanisa na shule ili kupewa msaada wa karibu.
Alisema kutokana na mafuriko hayo ya kiwango cha juu,  alichosema kiliikumba kwa mara ya mwisho wilaya hiyo mwaka 1952, anaomba Watanzania, kampuni na asasi mbalimbali, kuwasaidia kwa hali na mali waathirika hao wa mafuriko.
Dk Mwakyembe ambaye pia ni Waziri wa Uchukuzi, alisema hayo jijini Dar es Salaam jana.
Alisema ukiondoa kaya hizo 235 zilizoathiriwa vibaya, kaya zingine 3,983 zenye wakazi 48,976 zimeathiriwa, ingawa si kwa kiwango kikubwa na kwamba kaya hizo pia zinahitaji msaada.
Alisema kwa kaya zilizoathiriwa vibaya na mafuriko hayo, Kamati ya Maafa ya Wilaya hiyo iliyo chini ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Magreth  Malenga, imeanzisha makambi 14 ambayo yapo katika shule zilizo katika maeneo ya miinuko na makanisa ili kuwapa huduma ya karibu.
"Tumeona kaya zilizoathirika zaidi tuzipe hifadhi, kama mnavyojua hadi sasa tumewapoteza ndugu zetu saba kutokana na mafuriko ambapo wanne tumewazika na wengine watatu bado tunawatafuta baada ya kusombwa na maji," alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kutokana na janga hilo, misaada ya hali na mali inahitajika, ambapo alisema kwa upande wa chakula zinahitajika tani 796 za vyakula vya aina mbalimbali, vitakavyotosheleza kwa muda wa siku 60, huku pia zikihitajika boti mbili za kusaidia kuwavusha wanafunzi wanaokwenda shule.
"Pia tunahitaji mahema 335, mablangeti 670 na vyandarua 670. Msaada mwingine tunaohitaji ni dawa za aina mbalimbali zenye thamani ya Sh milioni 22, ambazo zitasaidia kuwatibu wenzetu wanaokumbwa na magonjwa mbalimbali," alisema.
Aliishukuru  Wakala wa Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) Mkoa wa Mbeya, ambao wamechangia Sh milioni 10 ambazo tayari zimepokewa na Kamati ya Maafa ili kuwasaidia waathirika wa mafuriko hayo.
"Juzi pia tulifikisha maombi ya msaada kwa Kitengo cha Maafa cha Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini kama mnavyojua kitengo hiki kina mambo mengi kinayoshughulikia hivyo tunawaomba Watanzania wenzetu kutuchangia, wakati tukisubiri msaada kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.
"Tumefungua Akaunti ya Maafa katika Benki ya NMB Namba  60910003908 kwa watakaokuwa tayari kutuchangia fedha," alisema Mbunge huyo.

No comments: