MAELFU WASHIRIKI SHEREHE ZA KIHISTORIA MIAKA 50 YA MUUNGANO

Wakati nchi ikiadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Jakaya Kikwete amesema umekuwa wa mafanikio katika kipindi chote cha nusu karne.
Amesema ni vizuri ukalindwa, kuimarishwa na kudumishwa, huku akisisitiza kuwa Muungano huo na usalama wa nchi kwa pamoja vipo salama.
Aidha, amesema kufanikiwa kwa Muungano huo kufikia miaka 50 jana, kunatoa picha kuwa jambo jema, linapokusudiwa na watu wenye nia njema linaweza kufanikiwa.
Rais alisema hayo Dar es Salaam, alipoungana na maelfu ya watu wakiwemo Watanzania, viongozi wakuu wa mataifa mbalimbali na wageni waalikwa kutoka sehemu tofauti duniani kwenye Uwanja wa Uhuru, kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Muungano huo, jana.
Katika maelezo mafupi aliyotoa wakati akiwatambulisha wageni mashuhuri, walioalikwa katika shehere hizo, Rais alisema, "Tuna kila sababu ya kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Muungano huu, kufikia miaka 50 na kushuhudia mafanikio ya kuungana kwetu si kitu kidogo".
Kwa mujibu wake, uzoefu uliotokana na Muungano huo, pamoja na mafanikio yaliyosababishwa na kuungana kwa nchi hizo mbili, vinaonesha wazi kuwa hata Shirikisho la Afrika na la Afrika Mashariki linawezekana.
"Uzoefu wa mashirikisho tunaanza kuupata kwenye Muungano wa nchi mbili kama hizi, tunaona kuwa kuungana kuna mafanikio hivyo tuamini kuwa hata mashirikisho hayo mengine yanawezekana", alisema.
Wakati akitoa shukrani kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kwa kuhudhuria sherehe hizo, Rais Kikwete alimweleza kwa njia ya utani kuwa enzi za utawala wa baba yake, yaani Jomo Kenyatta, shirikisho halikuwezekana, na kwamba, anaamini kwa sasa litawezekana, kwa kuwa yeye (Uhuru) yupo madarakani.
Katika hatua nyingine, Rais aliwatangazia Watanzania kuwa nchi ipo salama na kwamba, kama wananchi wanaoipenda nchi yao, wanahitajika kuhakikisha usalama huo unadumu siku zote, kwa kuulinda na kuutunza Muungano.
"Muungano wetu na nchi yetu vipo salama. Lakini, napenda kuwakumbusha kuwa, pamoja na kuwepo kwa usalama huo, Muungano unastahili, kuendelezwa kwa kutunzwa, kulindwa na kuimarishwa", alisema.
Mbali na kuwashukuru viongozi walioweza kufika nchini kusherehekea pamoja na Watanzania, Rais alisema anafahamu kuwa wapo waliopenda kufika na kushindwa kwa sababu za majukumu mbalimbali.
"Hata hao ninawashukuru pia, na kama mwenzangu wa Sudani Kusini (Rais Salva Kiir) naye najua anashughulikia matatizo ya nchini mwake. Nina imani kuwa matatizo yanayoikabili nchi yake yatakwisha na watu wataendelea kuwa salama," alisema.
Sherehe hizo za Muungano wa kihistoria Afrika, zilifana, kutokana na kupambwa kwa shamrashamra za kila aina yake.
Ukiachilia mbali michezo, burudani na maonesho ya kijeshi, Uwanja na Uhuru uliokuwa umefurika umati ulikuwa umepambwa kwa mabango yenye maneno “Utanzania Wetu ni Muungano, Tuulinde ni Muungano Wetu, Nusu Karne ya Uhai wa Taifa Letu”.
Mabango mengine yalikuwa na picha za Waasisi wa Taifa hili, Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume na bendera za  mataifa mbalimbali.
Rais Kikwete alipowasili majira ya saa 4:17 akiwa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange katika gari la wazi, akiongozwa na msafara wa pikipiki, alipokewa kwa nderemo na vifijo kutoka kwa wananchi na wageni, waliokuwa katika majukwaa kuzunguka uwanja huo.
Baada ya kushuka katika gari, Rais Kikwete alipokea salamu kutoka kwa askari wa vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama nchini, na baadaye kupigiwa wimbo wa Taifa, kabla ya kwenda jukwaa kuu alikosalimiana na viongozi na wageni waalikwa kutoka mataifa mbalimbali.
Tofauti na ilivyozoeleka kwa miaka mingine, ambapo gwaride lilikuwa likipita kwa mwendo wa pole na mwendo wa kasi, kutoa heshima kwa Rais, safari hii walipita askari wa nchi kavu kwa mwendo wa haraka na mchakamchaka, gadi ya askari wanamaji na makomando.
Shamrashamra hizo, pia zilipambwa kwa maonesho ya kundi la makomando wa JWTZ, zana za kivita, askari wa miavuli, maandamano maalum  yakiongozwa na farasi wenye mafunzo, wawakilishi wa wananchi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, wananchi waliozaliwa Aprili 26, onesho la mbwa waliofunzwa, onesho la askari Magereza wanavyoweza kudhibiti wafungwa na mahabusu na halaiki.
Onesho la makomando lililoongozwa na Luteni Utawanga, lilivutia wengi kutokana na umahiri na ukakamavu wao.
Pia askari wa mwavuli, walionesha umahiri wao wa kushuka kutoka angani, hali iliyomsukuma Rais kuwaita jukwaani askari walioshiriki ili kuwapongeza.
Mvuto mwingine ulikuwa katika onesho la zana za kivita, kuanzia zinazotumiwa na askari wa Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Anga na Jeshi la Majini. Halaiki iliyoshirikisha watoto, nayo ilikuwa kivutio kikubwa.
Wageni mbalimbali walihudhuria, wakiwemo marais wa mataifa mbalimbali, mawaziri na wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali, za ndani na nje ya Afrika.
Wakati Watanzania wakiwa katika chereko za miaka 50 ya Muungano, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Watanzania wana kila sababu ya kusherehekea miaka 50 ya Muungano, kutokana na mafanikio yaliyopatikana.
Ameyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja kuimarika kwa hali ya usalama, ushirikiano na maelewano kwa wananchi wa pande mbili za Muungano.
Maalim Seif alisema hayo juzi katika hafla ya mkesha wa Sherehe za Miaka 50 ya Muungano kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Alisema miaka 50 tangu kuasisiwa kwa Muungano huo ni kipindi kirefu cha kujivunia, kwani kuna nchi nyingi za Afrika, zilijaribu kuungana, lakini zilishindwa baada ya kipindi kifupi cha miungano yao. Alitaka dosari za Muungano, zipatiwe ufumbuzi wa haraka.
Kutokana na sherehe hizo, Rais Kikwete amekuwa akipokea salamu za pongezi kutoka kwa viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kuhusu Muungano wa kihistoria wa Tanganyika na Zanzibar,  uliotimiza rasmi umri wa miaka 50. Miongoni mwa viongozi hao ni marais Barack Obama wa Marekani, John Dramani Mahama wa Ghana na Giorgio Napolitano wa Italia.Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyotolewa juzi Dar es Salaam, ilisema mbali ya marais hao, wengine waliotuma salamu za pongezi ni marais wa Singapore, Falme za Kiarabu (UAE) na Mfalme wa Thailand.“Watu wa Marekani wanaungana nami katika kutuma salamu za pongezi kwa Watanzania wanaoadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Tunaamini Muungano huu utazidi kudumu na kudumu, aidha Tanzania itaendelea kushirikiana vyema na Marekani,” amekaririwa Rais Obama katika salamu zake.

No comments: