MAELFU WAMIMINIKA KUMZIKA GURUMO KIJIJINI KISARAWE

Maelfu ya waombolezaji wakiwamo wanamuziki wa muziki wa dansi, waigizaji wa filamu na wasanii wa kizazi kipya walijitokeza kwa wingi kumzika mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Muhidin Gurumo.
Mzee Gurumo ambaye alifariki juzi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na maradhi ya shinikizo la damu, alizikwa kijijini kwao Masaki, wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani jana.
Baadhi ya waombolezaji walionekana wakiwa wameketi katika vikundi vikundi wakijadili mchango mkubwa wa gwiji huyo ambaye alianza kutamba kwenye muziki wa dansi tangu mwaka 1960 akiwa na bendi ya NUTA Jazz.
Kabla ya kuelekea Kisarawe, Rais Jakaya Kikwete alitembelea nyumbani kwa marehemu eneo la Makuburi kwenye kutoa mkono wa pole kwa familia ya marehemu.
Pia msiba huo ulihudhuriwa na viongozi kadhaa akiwamo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal na Mbunge mteule wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete.
Pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana na Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu.
Mbali na viongozi hao, pia msiba huo ulihudhuriwa na wanamuziki na wasanii kadhaa mashuhuri nchini na baadhi ya viongozi wa chama cha muziki wa dansi nchini akiwamo Mzee Kassim Mapili.

No comments: