LHRC YATAKA CHOMBO KUDHIBITI MASHARTI YA KUKOPA

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeiomba Serikali iunde mamlaka ya kudhibiti taasisi za mikopo, kutoa riba nafuu na masharti rahisi, wananchi wa sekta zisizo rasmi waweze kunufaika.
Imeelezwa kwamba baadhi ya  taasisi, zimekuwa si rafiki kwa wajasiriamali kwa kulenga zaidi kufilisi mali za dhamana, huku zingine hazijasajiliwa kisheria na zimekuwa zikitapeli wananchi.
Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Flaviana Charles  aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia umuhimu wa serikali, kudhibiti taasisi za kukopesha fedha.
Alisema zaidi ya kesi 26 kwa mwaka zimeripotiwa katika ofisi zilizopo Arusha,  juu ya utapeli na ukiukwaji unaofanywa na taasisi za mikopo.
Alisema Serikali kupitia Wizara husika, iweke utaratibu mzuri wa kusajili vikundi vya wajasiriamali, ambao wamejikusanya, wapatiwe mikopo kiurahisi.
‘’Watunga sera wanatakiwa kutunga sera mahsusi zitakazoweka misingi kwa sekta zisizo rasmi  kwani hatuna sera inayozungumzia sekta hiyo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania wote,’’ alisema Charles.
Aliongeza kwa serikali za mitaa kupitia halmashauri, wapewe mamlaka kamili ya kuvitambua vikundi vya wajasiriamali na kuwapatia hati ya utambuzi  kupata mikopo katika taasisi za mikopo.
‘’Tukiyafanya hayo, Serikali itaboresha mazingira ya wananchi waliojiajiri katika sekta zisizo rasmi, itaruhusu wananchi wengi hasa vijana na wanawake ambao hawana ajira kuingia katika sekta hiyo na kuongeza pato la Taifa,’’ aliongeza.
Alifafanua kwamba LHRC imeanzisha Mradi wa Kazi na Staha kwa wananchi waliojiajiri katika sekta zisizo rasmi kuwezesha kupata tija katika shughuli zao.
Alisema katika mradi huo, wamefanikiwa kunufaisha vikundi 36, kati ya hivyo na vikundi 20 vya wanawake na 16 vya vijana, kutoka vikundi 620 vya akinamama na vikundi 175 vya vijana.
Alisema wameweza kuwajengea uwezo wajasiriamali hao kwa kuwajengea uelewa juu ya haki za binadamu, haki na wajibu, taratibu za kisheria katika usajili na leseni ya biashara.

No comments: