LAKE OIL YATOA MISAADA KWA HOSPITALI TATU

Kampuni ya Lake Oil imetoa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya  milioni 11.3  katika hospitali tatu za halmashauri za manispaa  za Ilala, Temeke na Kinondoni.
Msaada huo kwa hospitali za Mwananyamala (Kinondoni), Amana (Ilala) na Temeke, unalenga kupunguza changamoto za utoaji huduma za afya katika hospitali za umma nchini.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na vya kujifungulia kwa wajawazito, viti vya kubebea na kukalia wagonjwa, mashine za kupima shinikizo la damu na taa za uchunguzi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Ackim Mwaikasu alisema msaada huo umetolewa wakati muafaka ikizingatiwa kwamba hospitali husika zinakabiliwa na ukosefu wa vifaa mbalimbali.
“Ni kutokana na ukweli huo ndio maana tunaona msaada wa Kampuni ya Lake Oil umefika kwa wakati mwafaka na tungependa kampuni nyingine pia ziige mfano huu,” alisema Mwaikasu.
Meneja wa Lake Oil, Khaled Mohamed, alisema kampuni yake inaamini msaada huo utasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na sababu nyingine zinazoweza kuzuilika.
“Tumegundua kuwa vifo vingi katika hospitali zetu vinatokana na sababu ambazo tunaweza kuzizuia...kama kampuni, tunafanya biashara na watu na furaha yetu ni pale tunapochangia katika kuboresha afya ya jamii inayotuzunguka,” alisema Mohamed.
Alieleza kwamba hospitali hizo zilichaguliwa kutokana na ukweli kwamba idadi kubwa ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam hupata huduma za afya katika hospitali hizo.
Kampuni hiyo ilisajiliwa nchini mwaka 2005 na kuanza shughuli za uuzaji mafuta  jijini Dar es Salaam Machi, 2006. Hivi sasa ina vituo 73 vya kuuzia mafuta nchini.

No comments: