KIWANDA EPZA CHAPATA MASOKO MAREKANI, UINGEREZA

Kiwanda cha nguo katika eneo la Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) jijini Dar es Salaam, kimepata masoko  Marekani na Uingereza ambako kinauza jeans na fulana zinazozalishwa.
Meneja Mkuu Msaidizi wa kiwanda hicho cha Tanzania Tooku Garments CO.LTD, Rigobert Massawe alisema hivi karibuni jijini Dar es Salaam kwamba  kiwanda hicho kinazalisha nguo hizo kwa ajili ya masoko ya nje.
“Hiki ni kiwanda kikubwa cha nguo na masoko yake yapo katika nchi mbili za Marekani na Uingereza,” alisema Massawe wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene aliyefanya ziara kiwandani hapo mwishoni mwa wiki.
Alisema kwa sasa wanatumia zaidi soko la Marekani na baada ya maboresho zaidi watauza katika soko la Uingereza.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, kiwanda kimeajiri Watanzania zaidi ya 800 na kuwa katika malengo ya kiwanda kufikia mwaka 2025 kitaweza kuajiri watu 15,000.
Naibu Waziri Mbene alihimiza wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwa wingi katika maeneo ya EPZA kwa faida yao na ya nchi kwa ujumla.
Alisema uwekezaji katika maeneo hayo una uwezo mkubwa wa kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa masoko ya nje na hivyo kukuza uchumi wa nchi kwa haraka.
“Maeneo haya yana fursa nyingi ambazo wawekezaji wanaweza kufaidika nazo...nawahamasisha waje kwa wingi na serikali itawasaidia kuweka mazingira bora zaidi,” alisema Mbene.
Alieleza kufurahishwa na kiwanda hicho kutoa ajira kwa Watanzania wengi. Kabla ya kufanya ziara katika kiwanda hicho, Naibu Waziri huyo alikutana na watendaji wa EPZA na kufanya nao mazungumzo.
Katika mazungumzo yao, aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nayo vyema katika kusukuma gurudumu la maendeleo.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Adelhelm Meru alisema mamlaka yake imedhamiria kuona uwekezaji unakua na kuchangia maendeleo ya nchi hasa kupitia viwanda.
Alisema Tanzania inahitaji wawekezaji ili kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea na kuwa mamlaka yake itaendeleza juhudi za kuvutia wawekezaji hao.
Alisema kati ya kampuni 113 zilizojenga viwanda kupitia EPZA, asilimia 44 ni za ndani, ambapo asilimia 14 ni ya ubia kati ya kampuni za ndani na ya nje na asilimia 42 ni za nje.
Ni katika wiki chache zilizopita ambapo EPZA ilitoa leseni mpya kwa kampuni mpya 13 ambazo zinatarajia kwa pamoja kuwekeza mtaji wa dola za Kimarekani milioni 62.2 na kutoa ajira takribani 3,500 kwa Watanzania.

No comments: