KINANA ASISITIZA KATIBA MPYA NI LAZIMA

Licha ya 'madudu' yanayofanywa na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa  Katiba ya Wananchi (UKAWA), Katibu Mkuu CCM, Abdulrahman Kinana, amewataka Watanzania kuwa watulivu akisema ni lazima Katiba mpya itapatikana, huku akisisitiza watambue kuwa Katiba hiyo si mwarobaini wa matatizo yaliyopo sasa hapa nchini.
Kiongozi huyo alikuwa akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika, mjini hapa jana, ikiwa ni hitimisho la ziara yake ya siku 20 katika mikoa minne, Dar es Salaam, Rukwa, Kigoma na Katavi ya kukagua utekelezaji wa Ilani na kuimarisha chama hicho.
Katika mkutano alikuwa akizungumzia matukio yanayoendelea kutokea kwenye Bunge Maalumu la Katiba, ambapo aliwatoa hofu watanzania kuwa, hayazuii kupatikana kwa Katiba hiyo kama ilivyopangwa.
"Katiba nina uhakika tutaipata tena tutaizindua kwa shangwe, lakini naomba niwatahadharishe kuwa kupatikana kwa Katiba hii haimaniishi kuwa matatizo yetu yataisha hapo hapo, kila kitu kinakwenda kwa utaratibu wake, haina haja ya kutoana macho kama tunataka kitu kizuri," alisisitiza.
Alitolea mfano nchi ambazo zina Katiba bora duniani kama vile Afrika Kusini na Namibia ambazo hadi leo bado maisha ya wananchi wake yako vilevile kwa kuwa utekelezaji wa mwongozo huo unakwenda hatua kwa hatua.
Alisema kinachoendelea kwa sasa bungeni ni wazi kuwa baadhi ya watu kutoka vyama vya upinzani akili zao zimejikita katika uroho wa madaraka na ndio maana wanang'ang'ania mfumo wa Serikali tatu wakiwa na imani kuwa huenda wakapata madaraka.
"Nawaonea huruma kwa kuwa wanasubiria miujiza, hiyo ni sawa na kusubiri jua litokee Magharibi na kuzamia Mashariki," alisema Kinana.
Alibainisha kuwa chama hicho kimekuwa kikilaumiwa kuwa kinatawala maamuzi ya Bunge kutokana na wingi wa wabunge wake, jambo ambalo alikiri na kusisitiza kuwa wabunge hao hawakujipeleka wenyewe kwenye Bunge bali walichaguliwa na wananchi na maamuzi wanayotoa yanatokana na wananchi hao.
"Siku zote kura ya wengi ndio mshindi, sasa watu wanalalamika kuwa CCM wako wengi bungeni ni kweli, tena si bungeni tu hata huku mtaani tupo takribani milioni tano, mabalozi wa shina takribani milioni moja, na kila balozi ana watu 10 nyumba yake, ndio maana tunashinda ni kutokana na kuchaguliwa na kukubaliwa na wananchi," alisema Kinana.
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema yanayoendelea bungeni kwa sasa yasiwasumbue akili wananchi kwa kuwa chama hicho, kitahakikisha Katiba mpya yenye mtazamo na matakwa ya wananchi inapatikana.
Alisema kitendo cha Ukawa kuanzisha migogoro na kutoka nje ya Bunge ni kutafuta umaarufu kutokana na ukweli kuwa tayari walishalipwa posho ya siku sita hivyo kutoka kwao hakuwaathiri kimaslahi.
"Hawana lolote hawa, wanataka tu kukwamisha Katiba, hawana nia ya kuwezesha kupatikana kwa Katiba, wametoka juzi nje ya Bunge huku tayari mifuko yao imejaa posho, wanataka wakazitumie kwenye Pasaka, ikiisha watarudi, na ninawaambia kama kweli hawa wana uchungu kama wanavyodai, basi hawatorudi bungeni," alisema Nape.
Naye Mwenyekiti wa CCM, mkoa huo wa Katavi, Abdallah Mselem, alihoji juu ya kitendo cha baadhi ya wapinzani na wafuasi wao kutoa maoni yao juu ya mfumo wa Katiba wanaoutaka huku wakisingizia kuwa wametumwa na wananchi, jambo ambalo si kweli.
"Nawauliza wakazi wa mpanda huyu Lissu anayezungumza bungeni na mapovu kumtoka kuwa wananchi mmemtuma eti mnataka Serikali tatu mmemtuma kweli? Alikuja hapa mkamtuma awasemee, msikubali kuamuliwa," alisema Mselem.
Katikati ya wiki hii, wajumbe wa Bunge hilo wanaounda umoja wa Katiba ya Wananchi walisusa Bunge kwa kutoka nje ya ukumbi, wakidai kuchoshwa kubaguliwa na kudharauliwa.

No comments: