KIKWETE MGENI RASMI SIKU YA ALBINO

Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya tisa ya siku ya albino, yatakayofanyika Mei  5, mwaka huu.
Maadhimisho hayo yatafanyika kitaifa katika viwanja vya Mnazi Mmoja  jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafakari vikwazo vinavyosababisha tofauti ya umri wa kuishi kati ya albino na watu wengine.
Ofisa Habari wa Chama cha Albino Tanzania (TAS), Josephat Torner alisema hayo hivi karibuni, jijini Dar es Salaam wakati  akizungumzia maadhimisho hayo yenye  kauli mbiu ya "Haki ya Afya, Haki ya Uhai.’’
Alisema maadhimisho hayo ni moja ya mikakati ya kudai haki ya afya kwani kutotekelezwa kwa haki hiyo,  ni sawa na kutokidhi haki ya kuishi na kubagua sehemu ya jamii.
Kwa mujibu wa  Torner, Waziri wa Mambo ya Nje  na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe atafungua mkutano  wa kimataifa juu ya albino, utakaofanyika jijini Dar es Salaam. Mkutano huo wa siku moja, utafanyika Mei 3 mwaka huu.
Aidha, lengo la mkutano huo ni kupata sauti ya kimataifa kuutaka Umoja  wa Mataifa kuitangaza tarehe hiyo kuwa ya kimataifa kwa albino.
Alisema wataalamu kutoka Uturuki, KCMC, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Ocean Road watatoa huduma za  upimaji na tiba ya saratani ya ngozi.
Pia, watatoa msaada kisheria kwa watu wote utakaotolewa na Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada Kisheria (LHRC).

No comments: