KESI YA AKINA MRAMBA KUENDELEA TENA LEO

Kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, itaendelea kusikilizwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jana kesi hiyo ilitajwa kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa Mramba hata hivyo, Jaji Sam Rumanyika aliahirisha hadi leo kwa kuwa jopo la majaji watatu wanaosikiliza kesi hiyo halikukamilika.
Sababu nyingine ya kushindwa kuendelea kwa kesi hiyo jana ni kutokana na pande zote mbili katika kesi hiyo kutotimiza matakwa ya amri ya mahakama hiyo iliyotolewa Novemba 20,  mwaka jana.
Amri hiyo iliwataka kuwasilisha hoja za majumuisho ya jinsi ushahidi wa aliyekuwa Kamishna wa Kodi, Felesian Msigala utakavyopokewa mahakamani  ili kuunga mkono utetezi wa Mramba.
Hata hivyo Wakili wa Mramba, Hubert Nyange alidai kuwa aliwasilisha majumuisho hayo ingawa ilikuwa nje ya muda uliotolewa na Mahakama na alifanya hivyo ili kuokoa muda kwa kuwa aliona angesubiri mpaka kesi itajwe kisha aombe kuwasilisha hoja hizo nje ya muda angechelewa.
Jaji Rumanjika aliahirisha kesi hiyo hadi leo itakapotajwa na kuangalia ni jinsi gani amri hiyo itaweza kutekelezwa.
Majaji wengine wanaosikiliza kesi hiyo ni Jaji John Utamwa na Saul Kinemela. Mbali na Mramba, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja.
Wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Ilidaiwa kuwa walisababisha hasara hiyo baada ya kutoa msamaha wa kodi kinyume cha sheria kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.

No comments: