KANISA LA FULL GOSPEL LAKUMBWA NA MAFURIKO

Waumini wa Kanisa la Full Gospel la Mjini Ifakara , wilayani Kilombero, katika Mkoa wa Morogoro,  baadhi yao waliokolewa na boti la Halmashauri ya wilaya hiyo baada ya jengo lao kukumbwa na mafuriko ya maji ya mvua kwenye mkesha wa Pasaka.
Aidha wasafiri wanaotumia barabara ya Ifakara -Mlimba, wanalazimika kutumia  usafiri wa matrekta na magari maalumu yenye uwezo wa kuhimili tope na utelezi baada ya barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 150 kuharibiwa na mvua.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero, Yahya Anania , alisema hayo jana kutoka Mjini Ifakara akielezea hali halisi ya mvua za masika zilivyoathiri miundombinu ya barabara na makazi ya wananchi.
"Mvua kubwa zilinyesha usiku wa kuamkia mkesha wa pasaka...nyumba nyingi zilizingirwa na maji likiwemo Kanisa la Kakobe la Mjini hapa ambapo waumini wake walikuwa kanisani," alisema.
"Baada ya kupata taarifa za maji kuzingira Kanisa hilo tulilazimika
kutumia boti ya Halmashauri  ya Wilaya kwenda kuwatoa...baadhi yao walikiubali kupanda ndani ya boti, lakini wengine walikataa ... hapakuwa na madhara" alisema Katibu Tawala wa Wilaya.

No comments: