KAMPUNI ZA WATANZANIA ZAPIGIWA DEBE

Serikali imeombwa kuzijengea uwezo na  kuzipa kipaumbele kampuni za ujenzi za ndani katika miradi mikubwa kwa kuwa zina uwezo wa teknolojia na vifaa vya kisasa.
Hayo yalisemwa na Meneja Miradi wa Kampuni ya ‘Bharya Engineering and Contractors Ltd (BECCO), Jurie Wessels wakati wa ziara ya waandishi wa habari kukagua ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano kuanzia Gongo la Mboto hadi Chanika jijini Dar es Salaam.
Alisema  kwa muda mrefu miradi mingi ya ujenzi nchini imekuwa ikichukuliwa na kampuni kutoka nje ya nchi na kuziacha kampuni za ndani zikishindwa kupata nafasi hiyo kutokana na  kasumba iliyojengeka kwamba hazina uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa miradi mikubwa.
“Hivi sasa kampuni za ndani zina uwezo mkubwa wa kiteknolojia na umiliki wa vifaa vya kisasa zaidi zinapaswa kujengewa uwezo ili ifike mahali zabuni za miradi mikubwa ya ujenzi ikapewa kwa  kampuni za wazawa ili ziweze kuonesha uwezo wao,” alisema Wessels.
Alisema endapo kandarasi nyingi zikitolewa kwa wazawa zitasaidia katika kuziwezesha  kutoa huduma  bora  zenye ufanisi wa kiwango cha hali ya juu na hivyo kuziongezea kipato huku Serikali nayo ikiongeza mapato kutokana na kodi itakayolipwa na kampuni husika.
Ujenzi wa barabara hiyo ambayo ipo chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, unatarajiwa kukamilika mwanzoni wa mwezi ujao.

No comments: