KAMPUNI TISA ZA MAFUTA ZAFUTIWA LESENI

Bodi ya Wakurugenzi  ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imefuta leseni za kufanya biashara ya mafuta kwa kampuni tisa,  zinazojihusisha na biashara hiyo hapa nchini.
Uamzi huo ulifanywa jana katika kikao  cha Bodi ya Wakurugenzi kilichoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Ewura,  Simon Sayore kutokana na kampuni hizo kukiuka masharti ya biashara.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, kufutwa kwa leseni hizo, kumetokana na ukiukaji wa sheria na kanuni za biashara hiyo.
Ngamlagosi katika taarifa yake, alisema kampuni hizo zimefutiwa leseni kutokana na kukaa bila kuagiza mafuta kama leseni inavyowataka kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita tangu kupewa leseni hizo na Ewura.
Kampuni zilizofutiwa leseni ni Aspam Energy (T) Limited, MPS Oil Tanzania Limited, Panone Bulk Oil Importers Limited, Petcom (T) Limited, KMJ Tanzania Limited, Horizon Petroleum Company Limited, G.M and Company (T) Limited na Petronas Energy Tanzania Limited.
Mamlaka hiyo imeundwa chini ya sheria ya Ewura Sura Namba 414 ya Sheria za Tanzania.  Mamlaka hiyo ina majukumu ya kusimamia shughuli za udhibiti, kiufundi na kiuchumi  katika  sekta za Petroli, Umeme, Gasi Asili na Maji Safi na Maji Taka.

No comments: