KADHI WA DAR AMWAGA MACHOZI KUTUKANWA NYERERE NA KARUME

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na Kadhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Shehe Hamid Masoud Jongo alilazimika kumwaga machozi bungeni juzi kwa kile alichodai ni masikitiko yake kuona waasisi wa Taifa wanatukanwa na vijana wadogo wajumbe wa Bunge hilo.
Alisema waasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amaan Karume (wote marehemu) walitumia nguvu, akili, muda na utashi wao wote kulikomboa taifa mikononi mwa wakoloni na kuhakikisha undugu unadumishwa kwa kuungana hivyo si busara wazee hao wakatukanwa.
"Mtume anasema msiwatukane waliokufa, walishakutana na Mungu huko waliko, Mheshimiwa Makamu wa Mwenyekiti mimi nilikosa usingizi alipoghudhiwa Nyerere na Karume, wazee hawa wanatukanwa na watoto wadogo bila sababu yoyote," alisema Shehe Jongo huku akilia kwa sauti kubwa.
Jongo huku akilia, aliendelea kusema kwa mifano kuwa, Mji wa Dodoma umekuwa hivi ulivyo leo na kupata kuwepo kwa Bunge mjini hapa, uamuzi mkubwa wa kitaifa unafanywa hapa kutokana na juhudi za waasisi hao.
Baada ya kumaliza kulia, Shehe Jongo alihoji ujasiri wa kuwatukana, tena aliyezaliwa baada ya Muungano, anaupata wapi na kueleza kuwa, kuwatukana waasisi hao ni sawa na kuwatukana wazazi waliowazaa watu wenye umri rika na waasisi hao kwa kuwa walishirikiana nao.
"Haikubaliki hili, tutalipinga wazi wazi, mimi siko hapa kama mtu mwenye itikadi ya serikali tatu au nne, ila nitasema baadaye, lakini, kuwatukana ni makosa, nasaha yangu kwa Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), bora warudi, Sitta (Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba) kwenda kuwafuata ni ustaarabu," alisema Shehe Jongo.
Huku akiwafananisha Ukawa na watani wake katika mpira, timu ya Yanga, Shehe Jongo alisema, "Ukawa wametoka, nawafananisha na watani wangu Yanga wanagombana na taulo katika goli hawa Ukawa wangesubiri hapa hapa, huu ndio uwanja wa mpira."
Kuhusu muundo wa Serikali, Shehe Jongo alisema Watanzania shida yao si utitiri wa serikali bali linalowaumiza ni maisha yao na kutoa mfano kuwa, daraja liliposumbua wakati wa mvua hivi karibu, eneo (Ruvu) alikofika Rais Jakaya Kikwete wananchi hawakumwambia wanataka serikali tatu, bali msaada wa daraja kujengwa.
Alisema watu wanataka umeme vijijini, miundombinu bora ikiwemo barabara ili wanawake wajawazito wanaojifungua barabarani kwa ubovu wa barabara, na wengine kupoteza maisha, liishe.
Alisema katika mambo yanayohusu wananchi, hakupaswi kufanyika mizaha wala ushabiki na kusema kama watu wanataka ushabiki, Simba na Yanga zipo.
"Matusi, mipasho si vilivyotuleta humu, haya mambo ya kufyatua na nini, si sawa, wakati yanazungumzwa nilitamani kutoka nje lakini ikawa ngumu, inatia aibu," alisema.
Shehe Jongo na kueleza kuwa yeye pamoja na kwamba ni kiongozi wa dini ya Kiislamu, anaamini katika serikali mbili.
Alisema baada ya kusikia hoja za pande zote mbili na kutokana na mambo yaliyotokea, amekinaishwa na hoja ya serikali tatu lakini hajakinaishwa na ya serikali mbili kwa kuwa hakuna matatizo yatakayowapata Watanzania kwa kubaki na muundo wa serikali mbili.
Aliwatoa hofu Waislamu nchini kuwa Mahakama ya Kadhi ipo na si tatizo. Alisema yeye ndiye Kadhi Mkuu wa Dar es Salaam na wanawake wengi wamekuwa wakifika ofisini kupata msaada wa kisheria ikiwemo talaka na wamepata hasa wa umri wa kati ya miaka 25 hadi 30 lakini alisema mahakama hiyo haina utambulisho kisheria.

No comments: