JK KUZAWADIA WANAFUNZI BORA DARASA LA SABA

Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kutoa zawadi kwa wanafunzi na shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kuhitimu darasa la saba  na kidato cha nne kwa mwaka 2013 wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya elimu nchini Mei mwaka huu.
Taarifa ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa,  imesema pia Rais atatoa zawadi kwa halmashauri na mikoa iliyofanya vizuri katika mitihani hiyo ya mwaka jana wakati wa kilele cha Siku ya Elimu Mei 10.
Wakizungumza na mwandishi, baadhi ya wadau wa elimu walipongeza Serikali kwa uamuzi huo, ambao walisema utaleta tija katika elimu na utaharakisha matokeo makubwa sasa katika elimu.
"Uamuzi huu ni wa kupongezwa na umekuja wakati muafaka, tunaomba uwe endelevu kwani utakuwa chachu ya kukuza elimu mbali na kuzawadia shule na wanafunzi pia walimu wakuu wa shule zilizofanya vizuri watambuliwe na serikali kwani hatua hiyo itasaidia kuleta ushindani kwa walimu wengine katika kusimamia taaluma," alisema John Msangi.
Baadhi ya shule zilizofanya vizuri kwenye mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka jana ni Tusiime ya Tabata jijini Dar es Salaam iliyoshika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo hayo na kufanikiwa kufaulisha wanafunzi wote kwenda sekondari.
Mwanafunzi bora kitaifa kwenye matokeo hayo, Hemed Hussein aliyepata alama 243 alitoka shule hiyo ya Tusiime wakati wanafunzi kumi bora kitaifa kwa upande wa wasichana na kumi bora kwa wavulana wakitoka katika shule hiyo.
Mkoa wa Dar es Salaam ulishika nafasi ya kwanza kitaifa na wanafunzi 20 bora kitaifa walitoka shule ya Tusiime.

No comments: