IMEBAINIKA!! KARUME ALITANGAZA MUUNGANO NA TANGANYIKA MWAKA 1962

Imeelezwa kuwa wananchi wa Zanzibar walijulishwa mapema na Hayati Shekhe Abeid Amaan Karume kuhusu kuwapo kwa mpango wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Karume alisema mpango huo ungekamilika mara tu Uhuru wa Zanzibar, utakapopatikana kutoka kwa wakoloni.
Hayo yamesemwa na mwanasiasa mkongwe, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa (74) katika mahojiano maalumu kutimia miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hamad alisema kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Karume alikwenda Wete, Pemba na kuwaambia wananchi; “Tukipata uhuru tutaungana na wenzetu wa Bara na kuunda taifa moja lenye nguvu.”
Alisema mataifa ya Afrika, hasa ya jirani, yanatakiwa kuunganisha nguvu zao kwa ajili ya kujenga taifa lenye nguvu za kiuchumi na kuweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
“Nakumbuka kabisa Hayati Karume alikuja Pemba hapo Wete katika Uwanja wa mpira (Gombani) mwaka 1962 wakati wa harakati za siasa za uchaguzi wa vyama vingi na kutuambia tukipata uhuru tu, tutaungana na wenzetu wa Tanzania Bara kwa ajili ya kufanya Muungano, utakaounda  taifa lenye nguvu,” alisema Mberwa ambaye wakati wa Muungano,  alikuwa na umri wa miaka 24.
Alitaja sababu kubwa za kuwepo kwa Muungano huo ni kuimarisha umoja na undugu, uliopo wa asili wa makabila mbalimbali yaliyopo Unguja na Pemba pamoja na ulinzi wa usalama dhidi ya maadui.
Alisema wananchi wa Zanzibar na wenzao wa Tanganyika, kwa miaka mingi ni ndugu kwa hivyo njia pekee ya kuimarisha uhusiano wao ni kuunda Muungano.
“Unajua hapa Pemba kule Makangale wapo Wanyamwezi wengi, waliokuja hapa miaka mingi hata kabla ya Mapinduzi na sasa wanaishi vizuri sana wakiwa wamechanganya na wananchi wa Pemba,” alisema.
Aliongeza kuwa, hayo ndiyo baadhi ya matunda ya Muungano, ambayo Karume aliyasema mapema kuwa endapo nchi hizo zitaungana, wananchi watakuwa huru kuishi popote katika ardhi ya Tanzania na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kuijenga nchi, ikiwa pamoja na shughuli za kiuchumi na maendeleo.
Na hayo yanathibitishwa na ukweli kwamba, kwa sasa zaidi ya Wazanzibari 600,000 wanaishi na kufanya shughuli zao Tanzania Bara, wakati kutoka Tanzania Bara zaidi ya watu 120,000 wako Unguja na Pemba.
Mberwa alisisitiza kuwa, mbali ya kujenga umoja baina ya wananchi na kudumisha usalama wa nchi dhidi ya maadui, faida za Muungano zipo na zinaonekana waziwazi, ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati na ujenzi wa barabara za vijijini chini ya msaada wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mberwa ambaye amekuwa kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi Pemba tangu mwaka 1990 akiwa Mwenyekiti, aliutaja mradi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini (TASAF) ambao unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano umebadilisha maisha ya wananchi huku ukiibua miradi mingi ya wananchi, bila kujali ni upande gani wa Muungano.
Kutokana na mafanikio hayo, amezitaka serikali mbili, ya Muungano na ile ya Zanzibar kuharakisha kuzipatia ufumbuzi kero za Muungano ili kuziba chokochoko za wanaojaribu kudhoofisha Muungano huo, lakini pia kutoa fursa kwa wananchi kujikwamua kiuchumi.

No comments: