HOSPITALI YA TUMBI HAINA CT SCAN WALA X-RAY

Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi, ina ukosefu wa vifaa vya kupimia magonjwa mbalimbali,  vikiwemo CT Scan na X-Ray.
Pia, hospitali hiyo iliyopo wilayani Kibaha, inakabiliwa na uhaba wa madaktari na huduma ya maji.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Brayson Kiwelu wakati wa mafunzo ya uandishi wa habari za hali tete na migogoro, yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa waandishi wa habari wa mkoa huo.
Alisema matatizo hayo ni changamoto kubwa kwa Hospitali ya Tumbi.
Dk Kiwelu alisema vipimo vya CT Scan na X-Ray, vinapatikana kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Alisema hali hiyo inawapa shida kuwasafirisha wagonjwa hasa majeruhi kwa kutumia gari la wagonjwa, ambapo hutumia gharama kubwa kwa ajili ya mafuta.
"Hii kwetu ni changamoto kubwa, kwani baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakipoteza maisha wakiwa njiani kupelekwa hospitali hiyo ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya  vipimo hivyo na vingine, inafanyika hivyo licha ya hospitali hii kupandishwa hadhi na kuwa ya Rufaa, sawa na hospitali za mikoa mingine, ambazo zina vifaa kutokana na hadhi yake," alisema Dk Kiwelu.
"Mashine ya X-ray iko moja wakati mahitaji ni nne na mashine ya Ultra Sound ziko nne huku mahitaji yakiwa ni 10 ili kukidhi mahitaji ya wagonjwa na hadhi ya Hospitali ya Rufaa," alisema Dk Kiwelu.
Aliongeza kuwa hospitali hiyo ina upungufu wa madaktari 11, ambapo waliopo ni sita. Changamoto nyingine ni ucheleweshwaji wa madawa kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD).
Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku na ina vitanda 254 vya kulaza wagonjwa. Inasimamiwa na Shirika la Elimu Kibaha na ilianzishwa miaka zaidi ya 40 iliyopita.

No comments: