HATIMA YA KESI YA PINDA KUJULIKANA LEO

Hatima ya kesi ya kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda inatarajiwa kujulikana leo wakati Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itakapotoa uamuzi wa pingamizi la awali lililowasilishwa na upande wa mawakili wa Pinda pamoja na Mwanasheria Mkuu (AG).
Endapo Mahakama itakubali pingamizi hilo, kesi hiyo itaondolewa mahakamani na ikikataa, kesi itaendelea katika hatua ya usikilizwaji mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, akisaidiana na Jaji Augustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) dhidi ya Waziri Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Inadaiwa Pinda alivunja Katiba kutokana na kauli aliyoitoa bungeni, Juni 20, mwaka jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo, wakidai kuwa ni amri kwa vyombo vya utekelezaji wa sheria kuwapiga wananchi wakati wa vurugu.
Katika Pingamizi hilo, Pinda pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) wanadai kuwa kesi hiyo ni batili kwa kuwa walalamikaji na watu walioorodheshwa katika kesi hiyo hawana mamlaka kisheria kumfungulia kesi.
Aidha wanadai kesi hiyo imefunguliwa isivyo halali kwa kuwa inakiuka Katiba  na Sheria ya Mamlaka, Kinga na Haki za Wabunge, ya mwaka 1988 kwa kuwa Waziri Mkuu analindwa na Katiba Ibara ya 100 (1) na (2).

No comments: