EPZA KUPATA WAWEKEZAJI KUTOKA KOREA KUSINI

Tanzania kupitia Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), inatarajia kuanza kupata wawekezaji wengi kutoka Jamhuri ya Korea Kusini.
Matarajio hayo yanatokana na ziara, iliyofanywa hivi karibuni na wawekezaji katika mamlaka hiyo na kujionea maeneo maalumu ya uwekezaji na fursa zinazopatikana katika maeneo hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa nchi hizo mbili kuimarisha uchumi na uwekezaji endelevu.
Ujumbe huo ulijumuisha wafanyabiashara wakubwa kutoka kampuni 22 za nchi hiyo. "Wamekuja na ujumbe mkubwa sana na tunatarajia sasa kuanza kupata wawekezaji wengi kutoka nchi hii," alisema.
Pia, walioneshwa fursa zilizopo katika maeneo ya mamlaka, zikiwemo za kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani mazao ya Kilimo na madini kwa ajili ya masoko ya nje.
Fursa nyingine zilizotangazwa zilikuwa za ujenzi wa miundombinu ya nishati, maji na utoaji wa huduma mbalimbali katika maeneo maalumu ya mamlaka hiyo, yaliyopo katika mikoa 20 hapa nchini.
Balozi wa Korea nchini, Chung H aliyeongoza  ujumbe huo, alisema nchi yake ina uhusiano mzuri na Tanzania na ziara ya wafanyabiashara wa nchi yake inadhihirisha hilo.

No comments: