DUNIA YASIFU MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR

Rais Jakaya Kikwete amepokea salamu za pongezi kutoka kwa viongozi wa mataifa mbalimbali duniani kuhusu Muungano wa kihistoria wa Tanganyika na Zanzibar ambao leo umetimiza umri wa miaka 50.
Sherehe hizo zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa mataifa 38 duniani.
Miongoni mwa viongozi hao ni marais Barack Obama wa Marekani, John Dramani Mahama wa Ghana na Giorgio Napolitano wa Italia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nchini, mbali ya marais hao, wengine waliotuma salamu za pongezi ni marais wa Singapore, Falme za Kiarabu (UAE) na Mfalme wa Thailand.
“Watu wa Marekani wanaungana nami katika kutuma salamu za pongezi kwa Watanzania wanaoadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Tunaamini muungano huu utazidi kudumu na kudumu, aidha Tanzania itaendelea kushirikiana vyema na Marekani,” amekaririwa Rais Obama katrika salamu zake.
Naye Rais Mahama alimpongeza Rais Kikwete, akisema anashirikiana vyema na wananchi wake katika kuijenga Tanzania imara ili kujiletea maendeleo.
Anasema: “Mafanikio haya tunayaona chini ya utawala wako, nasi Ghana tunaiangalia Tanzania kama kioo cha muungano imara wa Afrika ulioasisiwa miaka 50 iliyopita, tunaamini kwa urafiki na ushirikiano baina ya Tanzania imara na Ghana utaendelea.”
Kwa upande wa Rais wa Italia, Napolitano ameelezea kufurahishwa na muungano huo, akisema unaipa faraja Italia wa kuendelea kushirikiana na Tanzania yenye mshikamano.
Katika salamu zake, Rais wa Falme za Kiarabu, Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan alimtakia Rais Kikwete furaha na maendeleo ya kasi wakati akisherehekea miaka 50 ya Muungano, katika kilele cha sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitakazofanyika leo jijini Dar es Salaam.

No comments: