DRC, TANZANIA WATAKA MSAADA KUNUSURU ZIWA TANGANYIKA

Serikali ya Tanzania na ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimetaka Jumuiya ya Kimataifa na marafiki wengine kutoa msaada wa hali na mali katika juhudi za nchi hizo kutekeleza mradi  unaohusisha ujenzi wa ukuta katika mto Lukuga ambao ndiyo pekee unaotoa maji kutoka Ziwa Tanganyika.
Waziri wa Maji wa Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe na mwenzake wa DRC, Bruno Kalala anayeongoza Wizara ya Maji na Umeme walitoa mwito huo hivi karibuni mjini hapa.
Mawaziri hao walikutana mjini Dodoma hivi karibuni kuongelea jinsi nchi hizo zinavyoweza kulinda rasilimali za Ziwa Tanganyika.
Mradi wa Lukuga unalenga kuzuia upungufu wa maji katika ziwa hilo. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na maofisa waandamizi wa serikali zote mbili.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya mawaziri hao, mkutano huo ulilenga kuweka mikakati ya pamoja na kutekeleza mapendekezo ya marais wa nchi hizo kuhakikisha kuwa ukuta unajengwa kwa haraka katika mto huo.
Mto Lukuga ndio pekee unaotoa maji ziwa hilo na kumwaga maji yake katika mto Congo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, pamekuwa na athari kubwa kutokana na kupungua maji ya Ziwa Tanganyika hasa katika miji ya Kigoma/Ujiji na Bandari ya Kigoma kwa upande wa Tanzania na bandari za Kalemie, Uvira na Moba kwa upande wa DRC.
Kwa mujibu wa mawaziri hao, kutekelezwa kwa mradi wa Lukuga ni hatua muhimu katika kutatua tatizo la kupungua maji katika ziwa hilo. Mradi huo utagharimu  dola za Kimarekani milioni 65.
Ziwa Tanganyika linatumika na nchi nne ambazo ni Burundi, DRC, Tanzania na Zambia. Burundi inamiliki asilimia na, DRC asilimia 45,  Tanzania asilimia 41 na Zambia asilimia sita.
 “Tumedhamiria kuhakikisha kuwa matumizi ya rasilimali ya ziwa hili yanakuwa endelevu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” ilisema taarifa hiyo.
Kupitia mkutano huo, mawaziri wamekubaliana kushirikiana katika ukusanyaji wa taarifa mbalimbali kuhusu rasilimali za maji, kufuatilia mienendo na kufanya ziara za kitaalamu kati ya nchi hizo. Pia ilikubalika kuwa serikali za nchi za Tanzania na DRC ziangalie jinsi ya kusomesha zaidi wataalamu wa masuala ya maji.

No comments: