CLEOPA MSUYA ATANGAZA RASMI KUACHANA NA SIASA

Rais Jakaya Kikwete juzi aliongoza mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro, katika sherehe za  kumuaga aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Cleopa Msuya, baada ya kutangaza kustaafu siasa.
Akizungumza jana  katika hafla iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya CCM  Wilaya ya Mwanga, Rais Kikwete alisema Msuya amekuwa kiongozi wa kuigwa na Watanzania pamoja na viongozi walio madarakani, kwa kutopenda kuendelea na madaraka kama ilivyo kwa wengine.
Alisema amekuwa mtu asiyetetereka hata pale alipokuwa akitoa kauli ambazo hazikuwapendeza baadhi ya watu.
"Wanamwanga mmefanya jambo la heri la kumuaga mzee wenu angali akiwa hai, tofauti na watu wengi huagwa wakiwa wameshatwaliwa dunia huku akimwagiwa sifa nyingi ambazo hawezi kusikiaÉhili ni jambo jema kutambua mchango wake katika taifa angali akiwa hai,Ó" alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema serikali itazidi kutimiza wajibu wake wa kuendelea kumhudumia, kumuenzi na kuthamini mchango wake katika nyanja mbalimbali za maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuchangia kukuza uchumi wa nchi katika kipindi chake alichotumikia taifa.
Pia Rais alimuomba Mzee Msuya kutumia muda wake wa mapumziko kuandika historia ya maisha yake katika utumishi wa umma na vipande  vya historia ya nchi, ili aweze kuacha hazina muhimu kwa taifa na uzoefu wake uweze kutumika.
Awali akitangaza kustaafu kwake Mzee Cleopa Msuya Mwenye umri wa miaka 83, alisema ameamua kustaafu shughuli zote za siasa ambazo amezitumikia kwa kipindi cha miaka 33, na atabaki kuwa mwanachama mwaminifu na mkereketwa wa CCM.
Msuya anastaafu kazi zote za siasa akiwa ametumikia taifa tangu mwaka 1955 hadi mwaka 2012 akiwa ameshika nyadhifa mbalimbali za uwaziri katika wizara tofauti, uwaziri mkuu,   makamu wa kwanza wa rais  pamoja na nyadhifa nyingine za juu za CCM.

No comments: