CCM YAZINDUA SHINA MARYLAND NCHINI MAREKANI

Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba amezindua shina la chama hicho Maryland, Marekani.
Uzinduzi huo ulifanyika juzi, ikiwa ni mwendelezo wa kuhakikisha wanachama wa chama hicho, wanakuwa katika mfumo mmoja wa kichama.
Akizungumza na Watanzania waliofika kwenye uzinduzi huo, Mwigulu alisisitiza umuhimu wa wana CCM, kujenga mazingira ya umoja na mshikamano, ikizingatiwa wako mbali na nyumbani.
"Umoja wenu ndio ngao yenu kwa hapa Marekani, naomba sana mshiriki kwenye Jumuiya zenu na mshiriki kwenye shughuli za pamoja zikiwamo hizi za kisiasa,” alisema.
Mwigulu alisema, “Haitakuwa vyema kufunga mashina na matawi ya CCM. Tutumie mashina haya kutuimarisha zaidi.”
 Aliwaelezea juu ya mchakato wa kutengeneza Katiba mpya, akisema kukosekana kwa utashi kwa viongozi wa kisiasa, kunasababisha katiba kutopatikana au kuchelewa kupatikana.
Aliomba Watanzania walioko nje ya nchi, kuacha kushabikia mambo yasiyokuwa na tija kwa taifa, kwa kuwa yatasababisha utengano.

No comments: