BUNGE KUTOA POLE SHILINGI MILIONI 44 MAFURIKO DAR NA PWANI

Bunge Maalumu la Katiba limeridhia kutolewa kwa posho ya siku moja ya wajumbe wote 629 inayofikia Sh milioni 44 kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mafuriko yaliyotokea wiki moja iliyopita mkoani Dar es Salaam na Pwani.
Hatua hiyo imetokana na Kamati ya Uongozi kuridhia hoja hiyo iliyotolewa na Mjumbe Profesa Mark Mwandosya bungeni humo akitaka wajumbe wakubali kutoa posho ya siku moja kuwasaidia waathirika wa mafuriko katika mikoa hiyo miwili.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu, alitangaza jana bungeni kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge kuwa, Kamati ya Uongozi imekubaliana na hoja hiyo ya Mwandosya.
Suluhu alisema kamati hiyo ilikaa jana asubuhi, pamoja na mambo mengine, ikaridhia hoja hiyo na posho itakayohusika ni ya kikao ya Sh 70,000.
"Kamati ya Uongozi imeridhia hoja ya Mwandosya kuunga mkono waliopata mafuriko Dar es Salaam na Pwani, hivyo posho ya shilingi elfu sabini itolewe ziende kusaidia serikali katika upande huo, kwa jumla ya wajumbe wote kiasi kitakachopelekwa ni Sh milioni 44," alisema Suluhu.
Mwandosya katika hoja yake, aliwaomba wajumbe hao kushirikiana na serikali katika kusaidia waathirika wa mafuriko kwa vitendo na kuwashawishi wajumbe wakubali kutoa posho yao ya siku moja kwa suala hilo.
Mafuriko makubwa yaliotokea jijini Dar es Salaam na Pwani yalisababisha watu zaidi ya 41 kupoteza maisha huku mamia wakijeruhiwa na kukosa makazi baada ya nyumba na mali zao kuharibiwa vibaya.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) wiki kadhaa zilizopita ilitangaza hatari ya kuwepo mafuriko kutokana na mvua kubwa kutarajiwa kunyesha katika kipindi cha siku tatu mfululizo katika maeneo mengi nchini hasa jijini Dar es Salaam.

No comments: