BINTI WA MIAKA 9 ATOBOLEWA MACHO BAADA YA KULAWITIWA

Kijana   Omary  Simon (30) anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Shinyanga  kwa tuhuma ya kumlawiti mwanafunzi wa darasa la pili (9)  anayesoma katika  shule ya Msingi Kitangili, Manispaa ya Shinyanga kisha kumtoboa macho kwa kutumia kitu chenye ncha kali na kumuacha porini akisota kwa muda wa siku mbili.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,  Evarist  Mangalla alisema tukio hilo lilitokea Aprili 20, mwaka huu majira ya saa 10;00 jioni katika kitongoji cha  Bugweto  nje kidogo ya mji  baada ya siku hizo aliokotwa na wanawake wawili.
Kamanda Mangalla alisema siku ya tukio mwanafunzi huyo ambaye anaishi na bibi yake Kata ya Ibinzamata alipewa Sh 500 na bibi huyo ili apande baiskeli kwenda kwa mama yake mkubwa anayeishi kata ya Ngokolo.
Mangalla  alisema alipofika katika kituo cha baiskeli zinazofanya biashara ya kusafirisha abiria maarufu kama daladala, alikutana na mtuhumiwa  Simon,  mwendesha  daladala ya baiskeli  ambaye alimpeleka katika pori dogo lililoko katika Kitongoji cha Bugweto na kumlawiti na kisha kumtoboa macho kwa kitu chenye ncha kali na kumtelekeza katika eneo hilo bila ya msaada.
"Tangu mwanafunzi huyo atoweke kwao Aprili 20, alikuja kuokotwa Aprili 22, mwaka huu majira ya saa 4;00 asubuhi na wanawake wawili na kumpeleka katika kituo cha Polisi ambao walimpeleka hospitali  ya mkoa  hadi sasa anaendelea kupata matibabu," alisema  Mangalla.
Kamanda Mangalla alisema mtuhumiwa tayari amekwishakamatwa  na jeshi la polisi hivyo  atafikishwa mahakamani  wakati wowote na iwapo atapatikana na hatia  ili kuweza kujibu shitaka hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari  bibi wa mwanafunzi  huyo alisema amefungua  kesi katika Kituo Kikuu cha Polisi  jalada lenye kumbukumbu namba SHY/RB/2098/2014 mara baada ya kuhisi mjukuu wake amefanyiwa kitendo hicho kutokana na hali aliyonayo.
Imeripotiwa kutoka Kibaha kuwa, Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Husna Iddi (16), mkazi wa Tarafa ya Vikindu, Kata ya Kisemvule wilaya ya Mkuranga kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mumewe baada ya kudaiwa kumvuta sehemu zake za siri.
Inadaiwa kuwa wanandoa hao walikuwa na ugomvi wa kimapenzi, hali iliyosababisha ugomvi na kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Ulrich Matei alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na alimtaja marehemu kuwa ni Jumanne Mwarami (21).
Kamanda Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 24 mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku ambapo wakiwa nyumbani na mke wake kulijitokeza ugomvi kati yao kwa marehemu kumtuhumu mke wake huyo kuwa siyo mwaminifu katika ndoa yao na ana mahusiano na wanaume wengine nje.
"Baada ya kutokuwepo kwa maelewano kati yao na ugomvi huo kuwa mkubwa ndipo mke wake huyo alimshambulia na kumvuta mume wake sehemu zake za siri, hali iliyosababisha kupoteza maisha wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga," alisema Kamanda Matei.

No comments: