BAJETI KUU 2014/15 KUSOMWA BUNGENI JUNI 12

Bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15 inatarajiwa kusomwa Juni 12, mwaka huu kwenye Bunge la Bajeti linalotarajia kuanza mkutano wake Mei 6 hadi Juni 27, mwaka huu mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana bungeni, Ofisa Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya  alisema ratiba hiyo imepangwa kufuatia mabadiliko ya mzunguko wa bunge hilo yaliyofanywa mwaka jana ili kuendana na mabunge mengine ya Afrika Mashariki.
Mwandumbya alisema kwa ratiba hiyo, kamati za kudumu za Bunge hilo zinaanza kukutana Aprili 28 hadi Mei  4, jijini Dar es Salaam ambapo kamati zote za kisekta pamoja na majukumu mengine zitapitia masuala yote yaliyojitokeza wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema wabunge wote watakutana Aprili 30, mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea mapendekezo ya mpango, kiwango na ukomo wa Bajeti ya serikali ya mwaka 2014/15 kama ambavyo kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge mwaka 2013 zinavyosema.
alisema kamati zisizo za kisekta zikiwemo Kamati ya Bajeti, Kamati ya Masuala ya Ukimwi, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), zitaendelea na utekelezaji wa majukumu yao kama yalivyoainishwa katika kanuni za Kudumu za Bunge.
“Tofauti na kamati nyingine, Kamati ya LAAC, zitaanza kazi mapema ambapo zilitakiwa kuwasili Dar es Salaam jana na kuanza kazi zake kesho”, alisema Mwandumbya.
Aliongeza kazi za kamati zitamalizika Mei 4, mwaka huu  na kwamba bunge la bajeti litakapoanza, linatarajia pia kupitisha mapendekezo kwamba liwe linakutana kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana, kisha kuendelea jioni saa kumi hadi saa mbili usiku, ikiwa ni pamoja na siku ya Jumamosi.

No comments: