BABA AUA BINTI YAKE KWA KUPALILIA VIBAYA SHAMBA

Mkazi wa Kijiji cha Ng'ereng'ere Kata ya Nyamaraga wilayani Tarime katika Mkoa wa Mara, Michael Bokoyo (64)  anatuhumiwa kumuua binti yake mwenye umri wa miaka 10 kwa mpini wa jembe akimtuhumu kupalilia shamba vibaya.  
Mtoto aliyeuawa ni Neema Michael  aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika  Shule ya Msingi Ng'ereng'ere  kwa kumpiga na mpini akimtuhumu wa kuacha magugu shambani.
Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Justus Kamugisha alisema kuwa tukio hilo ni la Aprili 17 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kamanda, baba huyo mzazi  alikwenda kukagua shamba lake la mahindi ambalo watoto wake walikuwa wakipalilia.
Inadaiwa alikuta nyasi ambazo Neema hakuzing'oa ndipo alimnyang'anya jembe na kumpiga nalo kichwani upande wa jicho la kulia.
Kamanda alisema mtoto alipata jeraha kubwa lililotoa damu na kusababisha mtoto kuzidiwa. Hata hivyo inadaiwa baba yake aligoma kumpeleka hospitali na Aprili 18 mtoto huyo alifariki dunia kwa kukosa msaada wa matibabu.
Mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.

No comments: