ASKOFU AKEMEA UNABII WENYE NIA MBAYA BUNGENI

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Dodoma, Gervas Nyaisonga, ameongoza Ibada ya kuombea Bunge Maalumu la Katiba bungeni humo, ili Mungu awezeshe wajumbe wa Bunge hilo kuwawakilisha Watanzania vyema.
Ameongoza Ibada hiyo jana wakati leo Bunge hilo likitarajiwa kuahirishwa na kwa mujibu wa Katibu wa Bunge Maalumu, Yahaya Khamis Hamad, Bunge hilo litaitwa tena mwanzoni mwa Agosti.
Nyaisonga katika mahubiri, amesema katika mchakato wa kupata Katiba, unabii mbalimbali umetolewa na wengine wakitabiri kuhusu mwisho wa mchakato na kutaka unabii wowote, bila kujali utatimia au la, usitumiwe kwa njia mbaya.
"Ninyi kama wawakilishi wa Taifa, mmetumwa kupasha habari za matumaini, furaha, na si ninyi pekee mmeitwa hivyo, bali hata sisi sote, si Wakorintho wala Wayahudi, bali sote," alisema Askofu Nyaisonga katika Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa dogo la bungeni mjini hapa jana.
Kuhusu unabii wa mchakato, alisema katika kazi ya wajumbe inayoendelea bungeni hapo, unabii mbalimbali umekuwa ukitolewa.
"Watu wametabiri hata mwisho wa mchakato, unabii usiwe na hatia kutimiza Mungu anavyotaka," alisema.
Katika kufafanua hilo huku akitoa mifano katika  Maandiko Matakatifu, Askofu Nyaisonga alisema wakati wa Yesu Kristo, unabii ulitolewa kuhusu yeye (Kristo) na Yuda Iskarioti
alipopokea fedha kumtoa Yesu auawe, baadaye alisikia hatia na hata Wayahudi waliomkataa Yesu walisikia hatia.
Alisema kwa nabii yeyote, kusudi la Mungu linapaswa kutimia katika njia sahihi na kutohalalisha dhambi kwa sababu fulani bali aliwataka wajumbe na Watanzania kwa ujumla, kuepuka dhambi, kuitikia mwito wa toba na kuhakikisha historia Mungu aliyowapa Watanzania, inakamilika vizuri.
Awali, Nyaisonga aliwapongeza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kwa kuwa na ujasiri na kukubali mwito na dhamana kubwa ya kutunga Katiba kwa niaba ya Watanzania na kutumia nafasi yao, kuhakikisha wanahubiri habari njema.
Katika Ibada hiyo, Askofu Nyaisonga pia alizindua Jumuiya mpya ya Bunge ya Mtakatifu Thomas Moore na kuwasimika viongozi wa jumuiya hiyo pamoja na kubariki jengo la Bunge la Kanisa dogo, wajumbe na waumini wengine waliohudhuria Misa hiyo.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ni Joseph Selasini ambaye mbali na kuwa Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba pia ni Mbunge wa Rombo (Chadema).

No comments: