ASILIMIA 98 DARASA LA PILI HAWAELEWI WANACHOSOMA DARASANI

Tathmini ya msingi ya Taifa kupima uwezo wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa Darasa la Pili,   imebaini kuwa asilimia 98 ya wanafunzi wa darasa hilo nchini, hawaelewi wanachokisoma.
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, tathmini hiyo ilifanywa kwa baraka za wizara yake kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Marekani (USAID), ili kupata taarifa kuhusu hali halisi ilivyo kwa wanafunzi wa Tanzania, kumudu stadi za KKK wanapofika Darasa la Pili.
Akizungumza hivi karibuni katika Kongamano la Wazi Kuhusu Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu jijini Dar es Salaam, Dk Kawambwa alisema tathmini hiyo ilifanywa na asasi ya Research Triangle Institute (RTI) ili kupima kitaifa stadi za KKK. 
"Upimaji huu ulifanyika katika halmashauri 20, shule 200 kwa wanafunzi 2,214 wa Darasa la Pili na ulitumia zana zilizojaribiwa na kuthibitishwa kimataifa za Tathimini ya Awali ya Kusoma (EGRA), Tathimini ya Awali ya Kuhesabu (EGMA) na  Halihalisi ya Menejimenti ya Shule na Uwezo wake Kutoa Matokeo Yanayohitajika (SSME).
"Upimaji huo umetuwezesha  kupata taarifa kuhusu hali halisi ilivyo kwa wanafunzi wetu kumudu stadi za KKK wanapofika Darasa la Pili. Nimefurahi kuona kwamba shirika hili la RTI ni sehemu ya kongamano la leo na washiriki mtaweza kusikia watoto wetu wako wapi katika stadi za KKK," alisema Dk Kawambwa.
Tathmini hiyo ilipofanywa ili kufahamu uwezo wa kusoma na kuelewa kwa lugha ya Kiswahili, matokeo yameonesha kuwa ni asilimia nane tu ya wanafunzi wa Darasa la Pili walioweza kusoma na kuelewa, kwa kuwa asilimia 92 hawakuweza kusoma na kuelewa.
Asilimia 40 waliopewa kazi ya kusoma, hawakuweza kujibu angalau swali moja kwa ufasaha, linalotokana na walichosoma.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, wanafunzi hao wa Darasa la Pili walipimwa welewa wao katika stadi za msingi za hisabati, kwa kuzingatia mambo kadhaa.
Miongoni mwa mambo yaliyotumika kupima wanafunzi ni kujumlisha na kupunguza, maarifa ya maana (kutumia maswali), kulinganisha namba na mafumbo ya hisabati.
"Wanafunzi walifanya vizuri zaidi katika maarifa ya akili
(wanakumbuka) vitu, na hawafanyi vizuri katika maswali
ya kuelewa zaidi kwa kutumia maarifa yao ya kiakili.
"Matokeo ya tathmini ya EGMA nchini Tanzania,
yanabainisha kwamba ufundishaji wa hisabati unazama zaidi katika kukariri kwa vipengele, kanuni, na fomula.
"Licha ya kuwa ukariri wa vipengele, unaweza kuchangia kutoa mwelekeo kwa watoto kufahamu hisabati yao katika hatua za mwanzo kabisa za awali (kwa mfano Darasa la 1 na la 2), EGMA nchini Tanzania ilibainisha kwamba wanafunzi hawakuweza
kutumia maarifa yao waliyoyakariri, kujifunza hisabati tete zaidi na za muhimu katika hatua za juu," ilieleza tathmini hiyo.
Tathmini hiyo ilibainisha kuwa asilimia 92 ya wanafunzi, hawakuwa na kitabu cha kujisomea darasani cha Kiswahili, asilimia 97 ya wanafunzi hawakuwa na kitabu cha kujisomea darasani cha Kiingereza, na asilimia 90 ya  shule hazikuwa na  maktaba, ambazo wanafunzi wangetumia.
Asilimia 51 ya wanafunzi hao, walikiri kuwa na vitabu vya ziada vya kujisomea nyumbani, mbali na vitabu vya shuleni. Lakini ni asilimia 19 tu walikiri kutumia vitabu hivyo, kumsomea mtu kwa sauti kila siku.
Wakati suala la kujifunza kusoma linahitaji mazoezi na wanafunzi wanatakiwa kuwa na muda na kuwa vifaa vya kujisomea, tathmini hiyo ilibainisha kuwa katika kipindi kimoja cha dakika 30 cha somo la Kiswahili, wanafunzi walitumia dakika saba tu  kusoma.
Kuhusu mafunzo kwa walimu, ni asilimia 25 tu ya walimu waliohojiwa, waliwahi kupata mafunzo maalumu ya awali au wakiwa kazini ya jinsi ya kufundisha kusoma, kuandika na hisabati kwa wanafunzi wa shule ya awali.
Walimu waliripoti kwamba walichunguza ustadi wa wanafunzi, kwa kupitia mitihani ya majaribio ya kuandika na mitihani kwa jumla.
Hata hivyo, ni walimu wachache walioripoti, kutathmini ustadi wa wanafunzi kwa kutumia matokeo yanayojenga (continuous assessment) ili kuchunguza welewa wa wanafunzi katika kung'amua maudhui ya maagizo, kurekebisha ufundishaji wao ili ukidhi mahitaji ya wanafunzi, au kupanga mafunzo ya siku za usoni na shughuli za kujifunza.
Wakati Tanzania ikipiga vita tangu Uhuru dhana yoyote ya ubaguzi, inaonekana pengo kati ya walionacho na wasionacho, limeanza kuchangia ubaguzi hadi katika elimu.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, wanafunzi waliotoka katika familia tajiri, walionekana kufanya vizuri mara 15 zaidi ya wengine.
Hata walimu wakuu wa wanafunzi waishio katika maeneo ya kipato cha chini, walikuwa na matarajio ya chini kuhusu ustadi wa wanafunzi wao.
Asilimia 67 ya wanafunzi waishio katika maeneo tajiri, walikuwa na vitabu vya kujisomea nyumbani, jambo ambalo lilichangia katika ufanisi na mafanikio yao, huku kwa wanaoishi katika kipato cha chini, asilimia 39 tu ya wanafunzi hao waliripotiwa kuwa na vitabu hivyo.
Wanafunzi wanaoishi katika maeneo tajiri, ilibainika kuwa walikuwa na nafasi ya  kufanya mazoezi ya kusoma kwa nguvu nyumbani na kumsomea mtu nyumbani, jambo lililochangia  kuwa na mafanikio.
Akitoa maelezo ufundishaji wa KKK, changamoto zake na nini kinafaa kuwa suluhisho, Dk Leonard Akwilapo kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE), alisema masomo ya lugha na hisabati, ndio msingi wa kujenga stadi za KKK.
Alisema stadi hizo, husaidia ujifunzaji na welewa wa masomo mengine na hivyo masomo mengine hukazia tu ujuzi wa KKK.
Alionya kuwa udhaifu wa KKK kwa mwanafunzi ni chanzo cha kuchukia masomo, kufanya vibaya katika mitihani na hata kuacha shule.
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo, umuhimu wa ufundishaji wa KKK ulitiliwa mkazo tangu enzi za Ukoloni na lengo la elimu wakati huo, lilikuwa ni kupata wafanyakazi wachache kama makarani katika maofisi, viwanda na mashamba. 
Mfumo wa elimu wakati huo wa Ukoloni, kwa Darasa la Kwanza mwanafunzi alikuwa na masomo sita tu na ufundishaji wake ulikuwa kama ifuatavyo.
Kwanza somo la Hesabu kwa wiki, lilikuwa na vipindi vitano, pili kulikuwa na somo la Kusoma lililokuwa pia na vipindi vitano na tatu somo la Kuandika, lililokuwa pia na vipindi vinne.
Somo la Hadithi lilikuwepo na lilipewa vipindi vitano na somo la tano, lilikuwa Kazi za Mikono, ambalo lilikuwa na vipindi vitano pia na somo la mwisho likiwa Dini, lililopewa kipindi kimoja kwa wiki. Imeelezwa mafanikio yalipatikana ya kukidhi mahitaji ya Mkoloni.
Baada ya Uhuru, Serikali ilibainisha matatizo makubwa matatu ya Ujinga, Maradhi na Umasikini ambapo katika kupambana na Ujinga, ilitilia mkazo programu mbili; moja ufundishaji wa KKK shuleni na pili kuanzisha Kisomo cha Watu Wazima.
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo, mafanikio yalipatikana na yalitokana na mambo makuu mawili, ambayo yalikuwa moja; utoaji wa mafunzo kwa walimu kazini na pili uimarishaji wa mazingira ya kufundishia.
Programu hizo, zimeelezwa kwamba zilikamilisha kazi yake mwaka 1980 ambapo idadi ya masomo wakati huo kwa darasa la I Ð III, yalikuwa masomo saba na darasa la IV Ð VII, masomo 13.
Kwa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, masomo yalikuwa Kiswahili, Hisabati, Sanaa na Uchoraji, Kazi za Mikono, Sayansi Kimu na Afya, Elimu kwa Michoro na Dini.
Kwa darasa la Nne mpaka Saba, masomo yalikuwa masomo yalikuwa Kiswahili, Hisabati, English, Historia, Jiografia, Michezo, Sanaa, Kilimo, Sayansi, Dini, Sayansi Kimu na Afya, Kazi za Mikono na Siasa.
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo mafanikio hayo yalianza kufifia baada ya kutokea kwa uandikishaji mkubwa wa watoto wa darasa la kwanza.
Changamoto zilianza kujitokeza kwa  kutokea uhaba wa walimu na madarasa, kupungua kwa walimu waliopata mafunzo na hapo kukajitokeza tatizo la stadi za KKK kwa wahitimu wa darasa la VII.
Kujitokeza kwa changamoto hizo na zingine, kulisababisha Serikali iunde tume ikiwemo Tume ya Makweta (1980) na Tume ya Taifa ya Elimu  (1990).
Mapendekezo ya tume hizo pamoja na mambo mengine, yalitaka  masomo ya msingi yapunguzwe kutoka masomo 13 hadi 7. Masomo mapya yaliyopendekezwa ni Hisabati, Kiswahili, English, Sayansi, Stadi za Kazi, Maarifa ya Jamii na Dini.
Hata hivyo, Dk Akwilapo alibainisha kuwa idadi ya masomo, si sababu ya kuporomoka kwa elimu kwa kuwa katika nchi za Afrika Mashariki, Tanzania wanafunzi wana masomo machache zaidi.
Kwa sasa imeelezwa kuwa mwanafunzi wa darasa la Kwanza na la Pili, anasoma kwa wastani wa juu masomo tisa tu ambayo ni Hisabati, Kiswahili, English, Sayansi, Tehama, Stadi za Kazi, Haiba na Michezo, French (Chaguzi), Dini.
Kwa Burundi, darasa la Kwanza na la Pili, ni masomo 11, ambayo ni Mathematics, Kirundi, English, Kiswahili, French, Environment, Physical Education, Religious Education, Musical Expression, Human Training Education na Civics.
Nchini Kenya, mwanafunzi wa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, masomo pia ni 11, ambayo ni Math, English, Kiswahili, Creative Arts , Science, Social Studies, Physical Education, Mother Tongue, Life Skills Education, Kenyan Sign Language, Religious Education (CRE, IRE, Hindu Religious Education).
Nchini Rwanda, wanafunzi wa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, anasoma masomo kumi ambayo ni Kinyarwanda, Mathematics,  English, Social Studies, Sports, Religious Education, Music, Fine Art, Cultural Activities na Practical Work.
Uganda wao ni masomo tisa kwa mwanafunzi wa darasa la Kwanza mpaka la Tatu, ambayo ni Mathematics, Literacy I, Literacy II, English,  Creative, Performing Arts (Music, Art and Crafts),  Physical Education, Religious Education, Free Activity na Oral Literature.
Dk Akwilapo alishauri ili kupata suluhisho la kinachotokea,  mafunzo ya walimu vyuoni yaimarishwe katika ufundishaji wa KKK na matumizi ya zana anuai.
Pia, alipendekeza mafunzo ya walimu kazini, yanayotilia mkazo ufundishaji wa KKK yapewe kipaumbele.
Pendekezo lingine ni kupunguza idadi ya wanafunzi darasani, wasizidi 35 kwa darasa, ili walimu watoe msaada kwa kila mwanafunzi.
Viwango vya vyumba vya madarasa imependekezwa view na ukubwa unaoruhusu kufanyika kwa ufasaha kwa vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji.   
Msomi huyo kutoka Taasisi ya Elimu Tanzania, alipendekeza  vitabu bora vya kufundishia KKK, vipatikane na vitabu vya kiada, viwepo pia vitabu vya ziada vyenye mvuto kwa wanafunzi (hadithi za kusisimua).
Mazingira ya kujifunza na kufundishia yamependekezwa kuwa rafiki kwa wanafunzi ili kupunguza utoro wa wanafunzi, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za madawati na viti, chakula cha mchana, maji safi na salama, vyoo safi na salama vitendea kazi vingine wezeshi.
Upatikanaji wa zana anuai za kufundishia KKK umetajwa kuwa wa muhimu, zikiwemo kadi na chati za herufi za alfabeti, kadi za namba, picha, kadi za maneno na sentensi.
Viongozi wameshauriwa kuhamasisha walimu kutengeneza vifaa hivyo kwa kutumia malighafi rahisi na zinazopatikana katika mazingira yao.
Jamii pia imetakiwa kushiriki katika elimu, hasa wazazi na walezi ili watambue wajibu wao katika elimu za watoto.
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo, tafiti zimeonesha kuwa wazazi/walezi wanaofuatilia na kuwasaidia watoto wao kujifunza, huwasaidia kupata matokeo chanya.
Pia, shule zimetakiwa kuwa na viwanja vya michezo na walimu wa michezo, ili kuimarisha mazingira ya shule na kupunguza utoro.

No comments: