AJALI YA BASI YAUA WATU 10, YAJERUHI WENGINE 30

Watu 10 wamekufa  papo hapo na wengine 30 kujeruhiwa vibaya kutokana na ajali ya basi la Luhuye Express lililokuwa likitoka wilayani Tarime mkoani Mara kwenda jijini Mwanza jana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea  majira ya saa  5:11 asubuhi katika Kijiji cha Itimila wilayani Busega.
Alisema basi hilo lenye namba za usajili T 410 AWT liliacha njia na  kugonga nyumba  ya Lazaro Mbofu na kuibomoa yote na kisha kupinduka.
Kamanda alimwambia mwandishi kwamba miili ya watu 10 ilitolewa kwenye basi hilo na majeruhi zaidi 30 walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mjini Mwanza kwa matibabu.
“Hadi sasa (jana jioni) kuna maiti 10 zilizopatikana eneo la tukio na zaidi ya watu 30 wamejeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu, ila taarifa kamili nitaitoa baadaye juu ya watu waliokufa na waliojeruhiwa kwani sasa nimetuma askari wa usalama barabarani kufuatilia,” alisema.
Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Juma Ally mkazi wa kijiji cha Itwimila, alimwambia mwandishi kwamba waliona basi hilo likiwa katika mwendo kasi.
Baadaye aliona likipoteza mwelekeo na kutoka barabarani na kisha kupaa juu na kugonga nyumba hiyo kabla ya kupinduka.
“Niliona basi hilo lililokuwa likitokea Barabara ya Musoma kuelekea
Mwanza likiwa katika mwendo wa kasi na dereva nadhani alishindwa kulimudu,” alisema Ally.
Aliendelea kusema, “liliacha barabara na kupaa juu kisha kugonga nyumba likapinduka.”

No comments: