MHAMIAJI HARAMU AKUTWA NA LESENI NA KITAMBULISHO CHA KUPIGIA KURA...

Leseni ya udereva.
Baadhi ya wahamiaji haramu, wamekuwa wakitumia mbinu ya kupiga picha na viongozi wa juu wa Serikali na kuzitumia kama ‘kibali’ cha kukaa nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari na kuonya kuwa mbinu hizo zimebainika na hazikubaliki.
“Kuna watu wasio raia ambao wamekuwa wakipiga picha na viongozi… hiyo haitakuwa dawa, hata mimi niliingia katika mtego na raia wa India ambaye katika kusalimiana, alipiga picha kumbe ni mhamiaji haramu, mtu huyo tulimwondoa mara moja,” alisema.
Alitaka wahamiaji haramu waliojificha, kurejea kwao au kuhalalisha ukaaji wao nchini kwa kufuata utaratibu wa kimataifa.
“Tunawapenda sana majirani zetu na tunawapenda marafiki zetu, lakini watu wanaotaka kuishi nchini ni lazima wazingatie utaratibu wa kimataifa. Vivyo hivyo kwa Watanzania wanaokaa nchi zingine,” alisema.
Alisema wakifuata utaratibu wa kimataifa, watasaidia kuongeza usalama wa nchi kujua ina raia wa nchi gani na hata nchi zao, kujua raia wake walio nje ya nchi.
Alionya Watanzania wanaopokea na kuhifadhi watu wasiowafahamu, kuwa mbali na matatizo ya kisheria yanayoweza kuwakuta, lakini pia wanahatarisha amani ya nchi.
“Kila mtu anatakiwa kuwa macho na wageni ambao hawawafahamu hasa katika kipindi hiki ambacho usalama wa dunia uko shakani,” alisema.
Nchimbi alitolea mfano wa gaidi wa Kingereza, ambaye  aliishi nchini kwa kubadili majina na alipenya hadi kupewa kadi ya mpiga kura.
“Pamoja na kupongeza watendaji kwa kumkamata gaidi huyo, lakini ukweli tutakuwa  tunashangaza… mpaka huyo mtu kapewa leseni ya Tanzania na kadi ya kupigia kura?” Alishangaa.
Nchimbi pia alitaka viongozi wa serikali za mitaa nchini watimize wajibu wao wa kuhakikisha wanakuwa macho na wahamiaji haramu katika maeneo yao.
 “Sasa tutaanza kuulizana na kuchukuliana hatua na wenyeviti na watendaji wa mitaa, kwani haiwezekani eneo moja tukamate wahamiaji haramu 30 au 40 na kuwachukua wao tu, wanatakiwa kuwajibika kwa hili,” alisema.
Wakati huo huo, ugomvi wa wapenzi, umesababisha raia   wa Tanzania, Martina Pius, kutoboa siri kuwa baba mtoto wake, Fidele Ndayiragijimana (25) ni mhamiaji haramu kutoka Burundi.
Akisimulia kisa hicho jana, Kaimu Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dodoma, Naibu Kamishna Proches Kuoko, alisema kwa sasa Ndayiragijimana ambaye alikuwa akiishi kijiji cha Itiso wilayani Chamwino, anashikiliwa katika Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dodoma.
Kwa mujibu wa Kuoko, Ndayiragijimana alikuwa akiishi katika kijiji hicho tangu mwaka 2009 na katika mapenzi yao na Martina, walibahatika kupata mtoto.
Alisema Ndayiragijimana alikuwa akifanya kazi kwa mkulima  na amekuwa akijitambulisha kwa bosi wake kuwa mzaliwa wa Kigoma.
Kuoko alisema baada ya kusikia Operesheni Kimbunga imeanza, Ndayiragijimana alirudi Burundi akachukue pasipoti na kuingia nchini na kuishi kihalali.
Hata hivyo, Ndayiragijimana alipata hati ya muda ya Burundi, ambayo Kuoko alisema aliitumia kuingia nchini kupitia mpaka wa Manyovu, Kigoma na kupata kibali cha mwezi mmoja cha kuingilia  nchini.
Hata hivyo, kibali hicho kilimaliza muda wake Septemba 6 na alipaswa kurejea kwao, jambo ambalo hakulifanya na kuendelea kuishi kwa siri, mpaka  Martina alipofichua siri hiyo.
Mhamiaji mwingine aliyekamatwa ni Husna Zekwana (26), raia wa Uganda, aliyekutwa na mtoto wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja aliyeingia nchini akitoka Kampala kwa kupitia mpaka wa Horohoro, Tanga.
Ofisa Uhamiaji huyo alisema Husna alikutwa na hati ya kusafiria isiyo yake, bali alipewa na kondakta wa basi la Smart ili avuke na kisha amrudishie baada ya kufika  Dodoma.
Akizungumzia Operesheni Kimbunga Awamu ya Pili, Dk Nchimbi alisema wanapanga upya ratiba, lakini nguvu ya kamatakamata inaweza kupungua kwa asilimia 70.
Katika awamu ya kwanza, kwa mujibu wa Dk Nchimbi, wahamiaji haramu 12,604 walikamatwa na kati yao, Wanyarwanda ni 3,448, Warundi 6,125, Waganda 2,496, Wakongo 589, Wasomali 44,  Myemeni mmoja na raia wa India mmoja.
Alisema watuhumiwa 212 wa unyang’anyi wa kutumia silaha walikamatwa, pia mabomu 10 ya mkono, silaha tofauti 61, risasi 665 na mitambo miwili ya kutengeneza   magobori.
“Tulifanya msako hata katika hifadhi za Taifa ambako ng’ombe 8,226 walikamatwa na zaidi ya Sh milioni 32.5 kupatikana kama tozo kutokana na faini ya ng’ombe walioachwa katika hifadhi ya Taifa,” alisema.
Nchimbi alisema pia walikamata nyara za Serikali ikiwamo ngozi ya duma, mbili za swala na vipande 10 vya nyama vinavyodhaniwa kuwa nyara za Serikali. Pia walikamata mbao 2,105, magogo 86, bangi kilo 77 na vipande viwili vya meno ya tembo.
Kuhusu wakimbizi wa Burundi zaidi ya 200,000 ambao wako nchini tangu mwaka 1972, Nchimbi alisema kazi ya kutoa uraia kwa watu hao ilisitishwa.
Sababu ya kusitishwa, ni hatua ya baadhi ya wabunge na wakuu wa mikoa kukataa kuwapokea baada ya kutokea vitendo vya uhalifu maeneo ya Kaskazini.
“Pamoja na kuwa tulikubaliana na Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR), tulisitisha kazi hiyo na sasa Serikali inatafakari njia mwafaka kwa kuwa kama mpango huo ungeendelea, basi ingekuwa Serikali yenye kiburi,”  alisema.

No comments: