POLISI WA KIKE DAR ATIMULIWA KAZI KWA KUJIPIGA PICHA ZA UTUPU...

Kamanda Suleiman Kova.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemfukuza kazi askari wake wa kike, WP Amisa, aliyekuwa akifanya kazi kituo cha Polisi Magomeni kutokana na utovu wa nidhamu.

Kamanda wa Kanda hiyo, Suleiman Kova alisema jana hatua hiyo imefikiwa baada ya askari huyo kukiuka maadili ya Jeshi kwa kitendo chake cha kupiga picha za utupu zilizoonekana katika mitandao.
"Jeshi halitasita kumchukulia hatua askari mwingine atakayeonekana kukiuka nidhamu ndani ya Jeshi, na hii ni nchi nzima kama ilivyokuwa kwa askari huyo kwa kuwa wanaharibu sifa nzuri ya Jeshi la Polisi," alisema Kova.
Alisema baada ya uchunguzi wa muda mrefu hasa baada ya taarifa na malalamiko ya watu kuhusu askari huyo, Juni 7 Jeshi hilo lilimtia hatiani askari huyo baada ya kujiridhisha na mwenendo mzima wa picha katika mitandao hiyo.
Aidha, katika tukio lingine, Jeshi hilo linamshikilia mtunza bustani wa nyumba ya Jaji Engera Kileo, aitwaye  Philemon Laizer (27) mkazi wa Mikocheni 'B', Dar es Salaam, kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mfanyakazi wa ndani wa nyumba hiyo, Perpetua Mainab (30) raia wa Kenya.
Alisema Perpetua alikutwa amekufa baada ya kuchinjwa na kukatwa mkono wa kushoto na uchunguzi ulipofanywa ilibainika kuwa aliuawa na mtumishi mwenzake  katika nyumba ya Jaji na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote.
Katika hatua nyingine, Polisi Jamii wa eneo la Vingunguti, Dar es Salaam, wametibua mipango ya askari watatu wa Jeshi la Polisi ya kupokea rushwa ya Sh milioni 4 kutoka kwa mtuhumiwa ujambazi na kukamatwa.
Hayo yalitokea juzi baada ya polisi hao kushuhudia mpango huo na kupiga simu kwa Ofisa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam ambaye aliwezesha kukamatwa kwa askari hao ambao ni makoplo wawili na konstebo mmoja (majina tunayo).
Taarifa zilizopatikana ndani ya Jeshi hilo jana, zilisema askari hao wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Konstebo wa kikosi cha usalama barabarani, ambao juzi walimkamata mtuhumiwa wa ujambazi wa kutumia pikipiki maeneo ya Vingunguti, Dar es Salaam na kisha kumwomba rushwa hiyo ili wamwachie.
Chanzo chetu cha habari kilieleza kuwa mtuhumiwa huyo (jina tunalo) juzi alikuwa na gari ambapo walimsimamisha na kujifanya kumhoji kwa makosa ya usalama barabarani na kisha kumwomba rushwa.
“Mtuhumiwa huyo wanamfahamu na siku hiyo walipanga kumfanyizia na ndipo walipomsimamisha na kumpeleka kituo kidogo cha  Polisi Vingunguti na kukaa naye hapo kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 9 alasiri wakimlazimisha awape rushwa,” kilisema chanzo hicho.
Tukio hilo kwa mujibu wa taarifa kilishuhudiwa na askari hao wa Polisi Jamii ambao walilazimika kupiga simu kwa Ofisa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ambaye alituma kikosi maalumu na kwenda kukamata askari hao na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi.
Baada ya kukamatwa, polisi hao waliwekwa ndani huku mtuhumiwa akipelekwa nyumbani kupekuliwa na kukutwa na bastola mbili na sasa anashikiliwa katika kituo cha Polisi cha Buguruni.
Taarifa zinadai kuwa mtuhumiwa huyo alipata kushiriki uporaji wa Sh milioni 15 akiwa na pikipiki maeneo ya Temeke Mwisho.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alipohojiwa kuhusu tukio hilo, alimwambia mwandishi wa habari hizi: “Hayo ni masuala yetu ya Polisi na nidhamu ya ndani na si ya kuandikwa kwenye magazeti.”

1 comment:

Anonymous said...

Greаt webѕite. Рlenty of useful information here.
I'm sending it to several buddies ans additionally sharing in delicious. And of course, thanks in your sweat!

Feel free to surf to my webpage: hemroids ()