KIWANGO CHA UFAULU KUONGEZWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI...

Baadhi ya wanafunzi wa mojawapo ya shule za msingi nchini wakifuatilia masomo.
Serikali imetaja mpango kamambe wa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2015.

Pia imesema imebainika wastani wa asilimia 53 ya muda wa masomo hautumiki kufundisha wanafunzi hivyo kuwa chanzo kingine cha kushuka kwa elimu nchini.
Akisoma Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi  bungeni jana kwa mwaka wa fedha 2013/14, Waziri wa Wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa, alisema ili kuhakikisha ufaulu unaongezeka, wataalamu wa 'Kikundi Maabara ' cha Elimu walipendekeza mambo mbalimbali kwa wizara yake.
"Kufanya tathmini ya kitaifa ya uwezo wa watoto wa darasa la pili katika kumudu stadi za Kusoma, Kuhesabu na Kuandika (KKK) kabla ya kwenda madarasa ya juu.
"Kuzipanga shule katika makundi ya ubora kulingana na kiwango cha ufaulu katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi na kidato cha nne na kuzitangaza katika vyombo vya habari," alisema na kuongeza kuwa mapendekezo mengine ni kutoa mafunzo kwa walimu wa darasa la kwanza na la pili kuhusu ufundishaji na ujifunzaji fanisi wa stadi za KKK.
Pia alisema mapendekezo mengine ni kutoa mafunzo kwa walimu ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Kiswahili, Kingereza na Hisabati kwa shule za msingi na masomo ya Kiswahili, Kingereza, Hisabati na Biolojia kwa sekondari.
Mapendekezo mengine ni kuimarisha maslahi ya walimu, kutoa motisha kwa shule zitakazoonesha ongezeko katika kiwango cha ufaulu, kuimarisha miundombinu ya shule za sekondari 1,200 ifikapo mwaka 2014.
"Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa ruzuku uendeshaji katika shule za msingi na sekondari na kuendesha mafunzo kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari za Serikali kuhusu menejimenti na utawala wa shule," alisema Dk Kawambwa.
Waziri huyo alisema katika kuhakikisha mapendekezo hayo yanafanyiwa kazi, Wizara yake iliteua kikosi kazi kwa lengo kusimamia utekelezaji wa kila siku wa maazimio ya kikundi hicho kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
"Aidha, kikosikazi hiki kimeanza kazi kwa kushirikiana na Tume ya Mpito ya Rais ya kusimamia uwasilishaji wa matokeo ya utekelezaji wa maazimio ya vikundi maabara ambapo imebainisha maeneo ya kipaumbele yanayotakiwa kutekelezwa ndani ya miezi sita ili kufanikisha kupatikana kwa matokeo makubwa sasa," alisema.
Akifafanua kuhusu kikundi hicho, Dk Kawambwa alisema  kilihusisha wataalamu 34 kutoka idara za Serikali, sekta binafsi na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Alisema kikundi hicho kilijikita katika kubaini chanzo cha kushuka kwa ufaulu na kutafuta mbinu za kukabiliana nayo.
Alieleza kuwa maabara hiyo ilibaini sababu za kushuka kwa ufaulu na kutaja kuwa ni uhaba wa walimu hasa wa masomo ya Hisabati, Sayansi na Kingereza, mazingira magumu ya kufanyia kazi kutokana na ugumu wa kufika na ukosefu wa huduma za jamii.
"Utoro wa walimu na ufundishaji na ujifunzaji usioridhisha darasani ambapo ilibainika kwamba kwa wastani asilimia 53 ya muda wa masomo hautumiki kufundisha wanafunzi," alisema.
Sababu nyingine ni kutotiliwa mkazo stadi za KKK, uhaba wa vifaa vya kufundishia, kukosekana programu za mafunzo kazini ambazo zingewezesha walimu kukabiliana na mabadiliko katika mitaala na udhaifu katika uongozi na usimamizi wa elimu katika ngazi ya shule.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, mjumbe wa Kamati hiyo, Zabein Mhita alisema matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha nne yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na kutumika kwa utaratibu mpya wa usahihishaji.
"Kamati inaona kwamba haikuwa busara kutangaza matokeo hayo yanayotokana na utaratibu mpya wa alama bila ushirikishwaji mpana wenye kuzingatia athari ambazo zingejitokeza," alisema Mhita.
Pia alisema suala la lugha ya kujifunzia na kufundishia linaleta changamoto kubwa katika suala zima la utoaji wa elimu nchini.
"Kamati inaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti kupata ufumbuzi wa suala hili muhimu ili kuwa na Taifa lililoelimika na lenye maarifa ya kukabiliana na mazingira yake.
"Aidha, sera ya elimu iwe wazi katika suala la lugha ya kufundishia na kujifunzia kuanzia ngazi ya elimu ya awali mpaka chuo kikuu," alisema.
Akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani, Msemaji Susan Lyimo alisema mchakato uliobadili matokeo ya kidato cha nne hauna tija kwa Taifa na unarudisha nyuma nchi.
"Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri Bodi ya Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA),  kwamba kwa kuwa Serikali imelazimisha mabadiliko ya matokeo ya kidato cha nne kinyume na miiko ya weledi wake, basi ijiuzulu ili kulinda heshima yake ya utaalamu na weledi kwa kutoruhusu uamuzi wa kisiasa kuathiri utendaji wa kitaalamu.
"Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo watumie busara zao na kujipima kama kweli pamoja na majanga makubwa yaliyotokea katika elimu ambayo madhara yake yatadumu kwa vizazi vingi, wanastahili kuendelea kuongoza wizara hiyo," alisema Lyimo.
Mbunge huyo alisisitiza kwa Waziri Kawamba na Mulugo wakijiuzulu itawajengea heshima na kuonesha wanajali misingi ya utawala bora na pia kulinda heshima yao mbele ya jamii.
Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM), alisema ni vema Bodi ya NECTA na kamati ya kutunuku madaraja katika mitihani zikavunjwa haraka iwezekanavyo, kutokana na kashfa ya matokeo ya kidato cha nne.
Mbunge wa Ngara, Deogratius Ntukamazina (CCM) alisema pamoja na mambo mengine, elimu nchini inaporomoka kwa sababu baadhi ya walimu ni ‘vihiyo’ na matokeo ya mwaka jana ya kidato cha nne ni janga la kitaifa.
Hata hivyo, alisema hakubaliani na kufutwa matokeo na kupanga upya madaraja badala yake ni vema ingerudiwa badala ya kutoa uamuzi ambao unaonekana kama wa kisiasa.
Lakini alisema jamii yote inahusika kutokana na matokeo hayo kuanzia kwa wazazi, wanafunzi, walimu na Serikali.

No comments: