CCM YAPELEKEA WANACHAMA WAKE RASIMU YA KATIBA WAIJADILI...

Nape Nnauye.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeamua kuijadili Rasimu ya Katiba kuanzia ngazi ya matawi, wilaya na Taifa ili kupata maoni ya wanachama wake na kuweka msimamo wake.

Hata hivyo, kimesema maoni yatakayotolewa na wanachama yatapaswa kuzingatia maoni ya chama hicho yaliyotolewa mwanzoni mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Pia Kamati Kuu (CC) imeiomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya kwanza mpaka ya mwisho, ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato mzima hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), Nape Nnauye alisema uamuzi huo ulifikiwa juzi kwenye kikao cha CC iliyokutana kwa siku moja mjini hapa maalumu kupokea Rasimu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete.
"Kamati Kuu inaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi nzuri na kukamilisha kwa wakati. Imepokea Rasimu hiyo na kueleza kuwa ni ya kwanza ambayo inapelekwa kujadiliwa na wananchi kupitia mabaraza ya Katiba baada ya kukamilika hatua ya kutoa maoni.
"Kamati Kuu imekiagiza chama kijipange kujadili Rasimu hiyo ndani ya chama kama baraza la kitaasisi la Katiba na kutaka wanachama na wapenzi wa CCM wajitokeze kushiriki mabaraza hayo," alisema Nnauye.
Alieleza kuwa ushiriki huo wa CCM baada ya kupokea Rasimu umekusudia kushirikisha wanachama   matawini, wilayani, mikoani na Taifa.
Pia alieleza kuwa jumuiya za CCM ambazo ni za  Vijana (UVCCM), Wazazi na  Wanawake (UWT) nazo zimeomba kushiriki kama mabaraza ya Katiba na hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato huo.
CCM kama Baraza la Katiba la kitaasisi, itaipitia Rasimu kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni yake yaliyotolewa mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, wanachama wetu watashiriki kutoa maoni yao.
"Pamoja na kazi nzuri ya Tume, CCM inaiomba Tume kueleza vizuri mchakato mzima kutoka Rasimu ya kwanza mpaka ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato huo hasa baada ya Rasimu ya kwanza kutoka.
"Kamati Kuu inawasihi Watanzania kushiriki tena kutoa maoni kupitia mabaraza, Bunge Maalumu la Katiba kwa Rasimu ya pili na kupitia kura ya maoni kwa Rasimu ya tatu kwa amani, utulivu na kuvumiliana, ili hatimaye tupate Katiba nzuri ya nchi yetu kwa maslahi ya Watanzania wengi," alisema Nnauye.
Alipoulizwa kwa kuwa msimamo wa CCM wakati wa kutoa maoni mwanzoni mwa mchakato huo ni serikali mbili, lakini Rasimu iliyotolewa na Tume hiyo inapendekeza serikali tatu,  alijibu: "CCM ni taasisi, haifanyi mambo kwa watu wachache kujiamulia kama baadhi ya vyama vilivyofanya.
“Umesikia leo CUF, Lipumba (Ibrahim-Mwenyekiti wa CUF) na Katibu wake (Maalim Seif Shariff Hamad) kila mmoja anatoa msimamo wake kuhusu Rasimu, mwingine anasema serikali tatu, mwingine serikali ya mkataba.
"Lazima wenzenu wakifanya mambo ya hovyo muwaambie wajifunze na ndicho ninachokisema, kwamba wamekosea, suala hili si uamuzi wa Nape na watu wachache ni jambo la kushirikisha wanachama.
"Pia inashangaza baadhi ya wenyeviti wa vyama wanakurupuka na kutoa maoni ya vyama vyao bila kupitia vikao. Sisi CCM tunawapelekea wanachama wetu Rasimu waijadili, lakini pia tumewaeleza wazingatie maoni tuliyotoa mwanzo, wapime na watakachokiamua ndio msimamo wa CCM.
"Tunasema hatutachakachua maoni yatakayotolewa na wanachama wetu, ila tutakachofanya tutawaambia maoni yetu mwanzo kama chama ni haya, Rasimu imekuja hivi, mnasemaje? Sasa wao wataamua, ndiyo maana nasema tutaijadili Rasimu kifungu kwa kifungu, maana kuna mambo mengi, hivyo wanachama wanaweza kusema hili sawa, hili hapana," alisema Nnauye.
Kuhusu muda, alieleza watakwenda sawa na muda ambao Tume imejipangia, hivyo kupanga kwenye   matawi ichukue wiki moja, na maoni yapelekwe kujadiliwa na vikao vya wilaya na kisha mikoa na  hadi Agoti 31 watakuwa wamemaliza kujadili mpaka Taifa na kupata msimamo wa chama.
"Tumeagiza ngazi ya matawi wajadili kwenye mkutano mkuu wa tawi, kisha wilaya  halmashauri kuu ya wilaya ambao watachambua yale kutoka matawini, kisha halmashauri kuu za mikoa zitajadili na kuleta taifani kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC)," alisema Nnauye.
Alitamba kuwa CCM ina wanachama karibu milioni sita nchi nzima na inaongoza Serikali, hivyo lazima ifanye mambo yake kwa umakini mkubwa na kueleza kuwa wapo baadhi ya wana-CCM waliotoa maoni yao baada ya rasimu kutoka, lakini bado wananchi wameendelea kuvuta subira kusikia chama kitasema nini kwani waliozungumza mwanzo, hata kama ni wana CCM lakini hawakuzungumza msimamo wa chama bali maoni binafsi.
Rasimu ya Katiba Mpya iliyozinduliwa hivi karibuni pamoja na mambo mengine, ilipendekeza muundo wa serikali tatu na kuruhusu mgombea binafsi kwa nafasi mbalimbali, ikiwamo ya urais.
Pia ilipendekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais wa Tanzania maeneo tofauti ya utendaji wake, ukiwamo uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali.
Rasimu pia inataka Rais ashirikiane na mihimili mingine ya Dola katika uteuzi huo, huku ikiwataja mawaziri na naibu mawaziri, Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi kuwa uteuzi wao utakapofanywa na Rais lazima uthibitishwe na Bunge.
Inapendekeza pia Rais ashauriane na chombo kipya kitakachoundwa cha Baraza la Ulinzi la Taifa kuteua viongozi wa taasisi za ulinzi nchini na mgombea urais apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kwamba, kinga ya kutohoji matokeo ya uchaguzi mahakamani iondolewe.

No comments: