WABUNGE SASA KUAMUA WATAKAOPATA MIKOPO ELIMU YA JUU...

Cosmas Mwaisobwa.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo mipya, huku ikiwaachia wabunge kuamua idadi ya wanufaika.

Heslb imetoa mwezi mmoja kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu, pamoja na wanafunzi wanaoendelea kwa mwaka wa masomo 2013/2014, kuomba mikopo kuanzia kesho kutwa hadi Juni 30.
Wakati  katika mwaka wa masomo wa 2012/13, wanafunzi 94,703 ndiyo walionufaika na mkopo huo wa elimu ya juu, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi hiyo, Cosmas Mwaisobwa alimwambia mwandishi, kwamba kwa sasa haijajulikana ni wangapi watanufaika.
Idadi ya wanafunzi watakaonufaika na kiasi cha fedha kwa ajili ya mikopo hiyo, havijajulikana kutokana na kile Mwaisobwa alichosema ni mpaka bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, itakaposomwa Mei 27 mwaka huu.
“Bajeti ya Elimu bado haijapitishwa, hatujui kiasi kitakachopitishwa. Ikipita, ndipo tutaeleza ni wanafunzi wangapi watapata mkopo,” alisema Mwaisobwa.
Awali, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwaisobwa alisema mwombaji wa mkopo huo anapaswa kuwa na sifa ambazo zimetajwa katika  Sheria   ya mwaka 2004 ambazo ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania.
Sifa nyingine ni kupata udahili katika chuo cha elimu ya juu, kutokuwa na njia nyingine ya kugharimia elimu ya juu, kufaulu mitihani ya mwaka uliotangulia kwa waombaji wanaoendelea na masomo, pamoja na kuwa mhitaji.
"Bodi inasisitiza kwamba waombaji wa mikopo wazingatie muda uliopangwa na pia wafuate kwa umakini taratibu zote zilizoainishwa katika uombaji wa mikopo," alisema na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada ya muda uliopangwa kupita.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Mawasiliano wa Bodi, maombi yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia anuani ya Bodi ya http://olas.heslb.go.tz.
Mwaisobwa alisema vipeperushi maalumu vyenye maelezo ya jinsi ya kuomba mkopo kwa njia ya mtandao, vinapatikana kwenye vyuo vya elimu ya juu, ofisi za elimu za wilaya, watoa huduma za intaneti, Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo na ofisi za Bodi ya Mikopo ya Kanda.
Waombaji wapya wanatakiwa kulipa ada ya maombi ya mikopo ya Sh 30,000, huku wanafunzi walio katika mwaka wa masomo wa tano au wa sita, wakiendelea kulipa ada ya maombi ya Sh 10,000.
Wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu na nne ambao walilipa ada ya maombi ya Sh 30,000 katika miaka ya masomo ya 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012, hawatalipa tena ada hiyo ya maombi ya mikopo.

No comments: