CHADEMA KUMBURUZA KORTINI RC ARUSHA KUHUSU SAKATA LA LEMA...

Magesa Mulongo.
Siku mmoja baada ya polisi mkoani kumkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), sasa chama chake kinahaha kumnasua mbunge huyo  kwa kumgeuzia kibao Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo wakidai watamfungulia kesi mahakamani.

Katibu wa chama hicho mkoani hapa, Amani Golugwa, amethibitisha dhamira ya Chadema, akisema wanaandaa utaratibu wa kumfungulia mashitaka Mulongo kutokana na walichodai kauli zake za uchochezi kwa chama hicho na vitisho kwa  Lema ambaye bado anashikiliwa na polisi.
Akizungumza mjini hapa jana, Golugwa alisema wameanza kufuata taratibu za kumfikisha Mulongo kwenye vyombo vya sheria.
Alisema Mulongo amekuwa kikwazo kwao kwa kuwa si mara ya kwanza kutoa lugha za uchochezi dhidi ya Chadema na kwamba mara nyingine amekuwa akimtuhumu Lema kwa uongo.
Kutokana na mazingira hayo, alisema kama chama hawawezi kupuuzia hali hiyo, sababu itazidi kuwaumiza na huenda wakapachikwa kesi zisizowahusu.
“Hadi sasa  tumeshawasiliana na wenzetu ambao ni wanasheria wa Chadema na tutamfikisha mahakamani huyu RC (Mulongo) maana  kauli  zake ni za  kutupinga  na sisi zinatuchosha,” alisema
Akizungumzia suala la kukamatwa kwa Lema usiku wa kuamkia juzi, alisema mpaka sasa mlalamikaji katika kesi hiyo hakuna, lakini wanahofia vitisho vinavyodaiwa kutolewa na Mkuu wa Mkoa kuwa mbunge wao huyo `hatachomoka’ katika sakata la sasa, hivyo kupitia kwa mwanasheria wao wanajipanga kukabiliana na Mulongo.
Awali Wakili wa Lema, Humprey Mtui alisema  anashangazwa na kitendo cha  polisi kumvunjia heshima mbunge huyo kwa kumkamata mithili ya mtu wa mtaani.
Alisema kwa mujibu wa sheria, Lema alipaswa kuitwa na Polisi lakini kama angekataa, basi ndipo angeweza kuchukuliwa sheria kama hiyo lakini sio kwa kitendo cha polisi, walichokifanya cha kwenda nyumbani kwake na kumkamata.
Mtui alidai kuwa mbali na hayo pia hata haki za msingi kama vile kuswaki na kunywa chai, mbunge huyo ananyimwa na polisi, jambo ambalo ni ukiukaji mkubwa wa sheria ya mahabusu hapa nchini, ukilinganisha kuwa yeye bado ni mbunge na tena mwakilishi wa wananchi.
Alifafanua kuwa bado watakuwa na mbunge huyo na wataweza kufuata sheria za msingi, lakini kwa wale wote ambao wanamuonea mbunge huyo watachukuliwa sheria, ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani kwani hali za uoneaji dhidi yake zinaongezeka siku hadi siku.
Kwa upande wa Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM mkoani Arusha, Isack Kapriano amelaani tukio hilo na kuiomba polisi kuhakikisha uchunguzi wa suala hilo unafanyika.
Naye Mulongo alipoulizwa juu ya Chadema kutaka kumfungulia kesi, alisema; “Huo ni upotoshwaji na naviachia vyombo vya uchunguzi kuendelea na uchunguzi wa jambo hilo, ikiwemo Lema kudai mimi nimemtumia ujumbe mfupi wa maneno wa kumbambikiza kesi.
“Sina la kuongeza, vyombo vya usalama vipo na vinafuatilia mambo haya hivyo nasubiri vifanye kazi zao, ikiwemo madai ya Lema dhidi yangu kwa SMS’’.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas, mbunge huyo wa Arusha Mjini alikamatwa saa tisa alfajiri, usiku wa kuamkia juzi, nyumbani kwake na kufikia jana aliendelea kuwa chini ya ulinzi, akihojiwa kuhusiana na vurugu zilizotokea katikati ya wiki hii katika Chuo cha Uhasibu Arusha baada ya mmoja wa wanafunzi wake, Henry Koga (22) kuuawa na watu wasiojulikana. Anatarajiwa kufikishwa kortini kesho kuhusiana na tukio hilo.

No comments: