PAPA AGOMEA IKULU, ALALA NA KULA VYUMBA VYA WAFANYAKZI...

Papa Francis I.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ameendelea kuwa kiongozi wa matukio yanayopingana na watangulizi wake, ambapo sasa amekataa kuhamia katika makazi ya kifahari ya Papa.
Uamuzi huo ni muendelezo wa msimamo wake wa siku nyingi, kwani alipoteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires, Argentina, alikataa kuhamia katika kasri la Askofu.
Kwa hatua yake hiyo, amevunja utamaduni ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka mia moja iliyopita.
Pia atakuwa akijumuika kupata chakula na wafanyakazi wengine wa Vatican, katika chumba cha kulia chakula cha wafanyakazi wote, pamoja na viongozi wengine watakaomtembelea.
"Ameamua kuishi maisha ya kawaida katika jengo wanaloishi wafanyakazi wengine. Leo (juzi) asubuhi, aliwaeleza makadinali wenzake kwamba ataendelea kuishi nao kwa muda fulani," alisema Msemaji wa Papa, Federico Lombardi.
Tangu utawala wa Papa Pius X, mwanzoni mwa karne ya 20, kila Papa baada ya kuchaguliwa, wamekuwa wakiishi katika kasri la kifahari la Papa.
Kasri hilo lipo katika ghorofa ya juu, lenye vyumba zaidi ya 12 vikiwemo vyumba vya wafanyakazi, baraza na sehemu nzuri ya kuangalia mandhari ya Jiji la Rome.
Mpaka sasa haijulikani ni lini Papa Francis atahamia katika Kasri la Papa, lakini akiendeleza msimamo huo, Papa mstaafu Benedict XVI, atakuwa akiishi katika kasri la kifahari kuliko yeye.
Benedict XVI, ambaye ameamua kuishi maisha ya ufungwa; ya kusali binafsi, kuliombea Kanisa na kupata tiba, anaandaliwa kasri lake Vatican, ambalo litakuwa maalumu kwa matumizi yake ya ustaafu na wafanyakazi wake.
Tangu alipochaguliwa, Papa Francis amekuwa akiishi katika vyumba viwili vya Hoteli ya Domus Santa Marta, iliyojengwa na Papa Yohane Paulo II, karibu na Kanisa la Mtakatifu Petro.
Karibu nusu ya vyumba zaidi ya 100 vinavyofanana na anavyoishi Papa Francis katika hoteli hiyo, hutumiwa na wafanyakazi wa Vatican.
Hata hivyo, wafanyakazi hao hulazimika kuhama katika vyumba hivyo, kuwapisha makadinali wanaokwenda Vatican wakati wa kumchagua Papa na baada ya uchaguzi, hurejea katika vyumba vyao.
Lombardi alisema hawezi kusema Papa ataendelea kuishi katika vyumba hivyo kwa muda mrefu kiasi gani, na kudokeza kuwa: "Bado ni muda wa kuzoea mambo."
Papa Francis, ataendelea kutumia Maktaba ya Papa katika ghorofa ya pili ya jengo lenye Kasri la Kifahari la Papa, kwa ajili ya kupokea viongozi na wageni wanaomtembelea.
Pia ataendelea kujitokeza kila Jumapili, katika dirisha lililotumika na mapapa waliopita, kuhutubia mahujaji katika Viwanja vya Kanisa la Mtakatifu Peter.
Siku moja baada ya kuchaguliwa kwake, aliwatoroka walinzi wake waliokuwa katika gari la upapa la kifahari aina ya Limousine, lisiloruhusu risasi kupenya, na kuchukua gari la kawaida kwenda nalo katika hoteli ya kawaida alimofikia, katika barabara zenye harakati nyingi za kibiashara.
Katika Misa ya Jumapili ya kwanza tangu achaguliwe, kabla ya Siku ya Misa ya Uzinduzi wa Kiti cha Upapa Jumanne, Papa Francis alikwenda kuzungumza na watu waliokuwa wamesimama kwenye geti la Vatican, kushikana nao mikono na kuingia katikati yao.
Siku ya Misa ya Uzinduzi wa Kiti cha Upapa, ambayo ilichukuliwa kama kuapishwa, ingawa Papa haapishwi, Papa Francis alisimama kwa karibu nusu saa katika gari la wazi, akibusu watoto na kuwabeba na kuna wakati, alishuka kwenye gari hilo na kwenda kumbusu na kumbariki mlemavu aliyekuwa katikati ya watu wengi.
Ametajwa pia kuwa na tabia ya kuchelewa katika matukio, ambapo Jumapili iliyopita, mmoja wa walinzi wake alionekana kumwomba afanye haraka kutoka kwenye Misa, wakati yeye akiendelea kuzungumza na watu.
Akizungumzia kuhusu tabia na usalama wake, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye ni miongoni mwa makardinali walioshiriki katika uchaguzi wa Papa Francis, alisema kiongozi huyo ni lazima abadilike la sivyo ipo hatari.
Alisema Papa Francis ni kiongozi wa aina yake, wa kawaida kupitiliza, na ambaye anapaswa kutambua kuwa kwa nafasi yake lazima ana maadui, hivyo asiuamini kupita kiasi ulimwengu na kuishi maisha aliyoyaishi nchini kwake.
Kardinali Pengo alisema hayo wakati akijibu swali la mwandishi aliyetaka kupata maoni kuhusu usalama wa Papa Francis, kutokana na mtindo wake wa maisha kuwaumiza vichwa walinzi wake hivi sasa.
"Papa atapaswa kujirekebisha, unaweza kufikiria kwa mtu kama Papa Yohana Paulo wa II (marehemu), ambaye hakuna aliyewaza kama anaweza kuwa chukizo kwa mtu, kwa namna alivyowapenda watu na kuwa karibu nao, lakini alitaka kuuawa kwa risasi mwaka 1981, kwa hali ya ulimwengu ya sasa, Papa mpya anapaswa kubadilika," alisisitiza Pengo.
Hata hivyo alisema mtazamo wake huo ni dhana tu, lakini inayopaswa kuchukuliwa kwa umakini, kwani kwa nafasi yake, kiongozi aliyeonesha wazi kupambana na watu wanaowatesa masikini, ni wazi baadhi ya matajiri hawatampenda, watataka wamdhibiti asiendelee kupiga kelele kuhusu wanyonge.
"Huyu anakuja na lengo kuu la kupambana na wanaowakandamiza masikini, Papa Yohana Paulo wa II alipambana na ukomunisti, ambao ulikuwa ukiwakandamiza watu, na watu walimchukia, itakuwaje kwa huyu anayetaka haki ya wanyonge na masikini, ni wazi mabepari hawatampenda," alisema Pengo.
Hata hivyo, alisema si juu ya Kanisa kutoa mwongozo wa namna ya kumlinda Papa, kwa kuwa ndiye kiongozi wa dhamana ya juu kabisa, ila anaamini Vatican imejipanga kuhakikisha anapata ulinzi stahili lakini pia Mungu aliyemchagua ni wazi anamuwekea ulinzi wake.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa jina la Mtakatifu Francisco wa Asizi, ambaye alikuwa Balozi wa Amani Duniani na aliyewajali masikini, Pengo alisema Papa Francis amechagua kuwa Balozi wa Amani na analiombea pia Taifa la Tanzania kutokana na vuguvugu la uvunjifu wa amani. Amewataka waumini kumuombea kiongozi huyo.

No comments: