NDEGE ILIYOBEBA MASHABIKI LIGI YA MABINGWA ULAYA YAANGUKA NA KUUA...

Uwanja wa ndege wa Donetsk ambako ndege hiyo ilianguka wakati ikijaribu kutua kwa dharura.
Watu takribani watano wamekufa baada ya ndege iliyobeba mashabiki wa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya huko mashariki mwa Ukraine kuacha njia yake na kuvunjika vipande wakati ikijaribu kutua kwa dharura usiku wa kuamkia leo.
Ndege hiyo yenye injini mbili aina ya Antonov turboprop ilikuwa ikiwaleta abiria 45 na wafanyakazi katika ndege ndogo kutoka mji ulioko ufukwe wa Bahari Nyeusi wa Odessa kuelekea Donetsk - wengi wao wakiwa wanatarajia kuhudhuria pambano la Ligi ya Mabingwa kati ya Shakhtar ya nchini humo dhidi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.
Wizara zinazohusika na dharura, zilinukuliwa na shirika la habari la Interfax, zikisema ndege hiyo ilitoka kwenye mstari wa kutua katika uwanja wa ndege wa Donetsk ambapo mashuhuda walisema ilifunikwa kwenye ukungu mzito wakati huo. Ilipinduka na kuvunjika.
Mbali na watu watano waliothibitishwa kufa, wengine 12 wamejeruhiwa, wizara hiyo ilisema.
Andriy Shyshatsky, mkuu wa tawala ya mkoa wa Donetsk akizungumza kabla ya mtu wa tano kuthibitishwa kufa, alisema wengi wa abiria hao walikuwa wameokolewa.
"Mtu mmoja anaonekana kwenye mabaki ya ndege hiyo, lakini kwa sasa hatufahamu kama ni mzima ama amekufa. Tunamsaka mtu mwingine mmoja," Shyshatsky aliwaeleza waandishi wa habari.
Chanzo cha habari cha uwanjani hapo kilinukuliwa na Interfax kikisema mhudumu wa kike ambaye alikuwa mbele ya ndege hiyo hakuwa amehesabiwa.
Watu wote walisimama kwa dakika moja kwa ajili ya kuwakumbuka waliopoteza maisha wakati wa kuanza kwa mechi hiyo ya Klabu Bingwa Ulaya.
Hakukuwa na taarifa zozote kuhusu kwanini wafanyakazi wa ndege hiyo waliamua kutua kwa dharura. Lakini aliyenusurika kwenye ajali hiyo, aliyenukuliwa na Interfax, alisema ndege hilo ilishika moto angani ambapo uliweza kudhibitiwa.
Hii haikuweza kuthibitishwa mara moja na maofisa. 

Pambano hilo lilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

No comments: