MWANAMKE MSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA AFA AKIHOJIWA 'AIRPORT' DAR...

Uwanja wa Ndege ambako watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa tayari kwa safari ya Osaka, Japan.
Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Margret Temu (45) amekufa ghafla  baada ya kudhuriwa na pipi 64  za dawa za kulevya  alizomeza ili kuzisafirisha kwenda Osaka, nchini Japan akiwa na mwenzake.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP)  Deusdedit Kato alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo.
Kamanda Kato alisema tukio hilo lilitokana na kukamatwa kwa watu wawili kwenye Uwanja wa Ndege  wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa  katika harakati za  kusafirisha nje ya nchi dawa ambazo wanahisi kuwa ni za kulevya katika tukio lililotokea  Jumatano ya wiki hii.
Kamanda Kato alisema  Margret akiwa na mwenzake Allen Habibu Ally  (28) mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam walikamatwa na askari wa kike wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini ambaye hakumtaja  baada ya kuwatilia mashaka.
Kwa mujibu wa Kamanda Kato  askari huyo  alimtilia shaka Ally  na  ndipo alimfuata  na kuzungumza naye  ambapo  baada ya mtuhumiwa kubaini kuwa alikuwa ni askari alimshawishi ampatie  dola za Marekani 3,000 ili amwachie aendelee  na safari yake  ya Osaka, Japan.
Alisema  askari huyo wa kike ambaye jina lake limehifadhiwa kutokana  na taratibu za kazi zake alikataa ushawishi huo na kuamua kuwakamata  Ally na Margret  baada ya kubaini  kuwa  mienendo yao kiwanjani hapo ilionekana kuwa wanafahamiana na wako katika safari moja.
“Baada ya kukamatwa Margret na Ally , Polisi waliwahoji na Ally alikiri kumeza  pipi  75 za dawa hizo ambazo zinadhaniwa kuwa  ni za kulevya   lakini Margret alikataa katakata kumeza chochote  lakini  ghafla wakati mahojiano yakiendelea mtuhumiwa huyo alianza kutokwa na damu puani na povu mdomoni na wakati huo huo Ally pia alianza kutokwa na povu,” alisema  Kato.
Alisema kitendo hicho kiliwafanya polisi kuwakimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini Margret  alifariki kabla ya kufika hospitali wakati Ally alisalimika  baada ya kupatiwa matibabu.
“Baada ya mwili wa Margret  kufanyiwa uchunguzi na upasuaji mbele ya ndugu zake ambao polisi iliwapata kwa msaada wa maelezo yake yaliyokuwa kwenye  hati yake ya kusafiri alikutwa amemeza pipi 64,” alisema Kamanda huyo.
Alisema kwa upande wake Ally, mara baada ya hali yake kutengemaa siku iliyofuata  alirudishwa Polisi ambako alitoa pipi 69  kwa njia ya haja kubwa ambazo polisi wanadhani ndizo alizomeza. Alisema pipi hizo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kubaini ni aina gani ya dawa za kulevya.
 Aidha kutokana  na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na dawa hizo pamoja kugoma kushawishika  kuchukua hongo na kuonesha uadilifu  na uaminifu katika kazi yake, Kamanda Kato alisema Jeshi la Polisi limemzawadia askari  huyo Sh milioni tano ambazo ni sawa na kiasi cha dola za Marekani 3,000 ambazo alitakiwa kuhongwa na watuhumiwa aliowakamata.
Kwa mujibu wa Kamanda Kato kuwazawadia askari wa aina hiyo ni sera ya Jeshi la Polisi nchini  ambayo inaelekeza kutoa kiasi hicho  cha fedha kwa askari endapo inathibitika kweli alitaka kuhongwa na kuwataka askari wengine waige mfano bora ulioneshwa na mwenzao.

No comments: