MATOKEO YA KIDATO CHA NNE KUTANGAZWA KESHO...

Dk Shukuru Kawambwa.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema kwamba matokeo ya kidato cha nne yatatangazwa wiki hii kufuatia swali aliloulizwa kutaka kujua ni lini matokeo hayo yatatangazwa.
Dk Kawambwa alitangaza hilo pamoja na ajira mpya za walimu alipokutana na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Kufuatia kauli ya Waziri huyo, inamaana sasa matokeo hayo yatatangazwa si zaidi ya kesho (Ijumaa) hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba siku za kazi kwa ofisi za serikali zinaishia Ijumaa.
Alisema serikali haijachelewa kutangaza matokeo hayo kwani wanafunzi watajiunga na kidato cha tano Julai mwaka huu. “Hapo mtasema tumechelewa kivipi?
Mbali na hilo, Dk Kawambwa alisema Serikali imeajiri walimu 26,537, ambao wataanza kazi kuanzia Machi mosi mwaka huu, ikiwa ni mkakati wa kupunguza tatizo la walimu nchini.
Miongoni mwa walioajiriwa, walimu wa sekondari na vyuo vya ualimu ni 12,973, wakiwemo wenye shahada 8,887 na stashahada 4,086.
Walimu waliopangwa kufundisha shule za sekondari zilizo chini ya halmashauri ni 12, 893, wakufunzi wa vyuo vya ualimu 59 na walimu 21 wataenda kufundisha sekondari za mazoezi.
Walimu wa ngazi ya cheti walioajiriwa ni 13,568, ambao
wataenda kufundisha katika shule za msingi.
Katika mgawanyo huo, walimu 41 kati ya hao wataenda kufundisha katika shule za msingi za mazoezi, zilizo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na idadi iliyobaki watapelekwa kwenye shule zinazosimamiwa na Tamisemi.
“Idadi hiyo (walimu 26,537), inajumuisha walimu 188 wa elimu maalumu wenye shahada, ambao wamepangwa katika shule za sekondari na vyuo vya ualimu vinavyotoa elimu maalumu,” alisema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Dk Kawambwa alisema idadi ya walimu walioajiriwa mwaka huu wa fedha, imeongezeka kwa asilimia 11 sawa na walimu 2,630, ikilinganishwa na walioajiriwa mwaka uliopita.
Hata hivyo pamoja na ajira hizo mpya, idadi ya walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao wameajiriwa, ni walimu 2,037 tu, wakiwemo 904 wenye stashahada na 1,132 wa shahada.
Serikali ina ukosefu wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati 28,960, hivyo kuajiriwa kwa walimu hao kunafanya upungufu wa walimu wa masomo hayo ubaki 26,967.
“Idadi ya walimu tuliajiri ni asilimia 15 tu ya walimu wote mbao wameajiriwa, hivyo bado tuna upungufu mkubwa katika masomo hayo,” alisema Kamishna wa Elimu, Profesa  Eustella Bhalalusesa.
Waziri alisema kuwa kati ya walimu wa sekondari na vyuo walioajiriwa, walimu 1, 286 ni walioomba ajira serikalini kutoka katika soko la jira.
“Hawa ni tofauti na wale waliotoka vyuoni moja kwa moja,” alisema Dk Kawambwa na kuongeza kuwa walioajirwa, ni pamoja na walimu wa ngazi ya stashahada 841 na waliorudia mtihani mwaka 2012 na kufaulu.
Baada ya tangazo hilo, Dk Kawambwa amewaagiza walimu wote walioajiriwa, kuripoti katika vituo vyao vya kazi, kati ya Machi mosi hadi Machi 9 na wale watakaoripoti nje ya tarehe hizo, ajira zao zitakuwa zimefutwa.
Aliwataka kuripoti wakiwa na vyeti vyao halisi vya taaluma, cheti cha kuzaliwa pamoja na nakala zake, ili vihakikiwe na kukamilisha taratibu za ajira zao.
Kuhusu stahiki zao, Dk Kawambwa alisema wakurugenzi wa halmashauri na Katibu Mkuu wa Wizara, watawalipa
walimu wapya malipo stahili kwa mujibu wa nyaraka na miongozo ya Serikali, kuhusu waajiriwa wapya.
“Hili tutalisimamia ili kuhakikisha wanalipwa mshahara wao kwa muda stahiki na nawaomba walimu wote waripoti katika kipindi hicho tulichoagiza,” alisema Dk Kawamba.
Akiongezea juu ya suala hilo, Naibu Waziri, Philipo Mulugo, alisema watalipwa posho ya siku saba na sio 14 kama inavyodaiwa, lakini pia hawagharimii mizigo kwani wanaamini kuwa walimu wote wanatoka vyuoni.
“Mtu katoka chuoni ana mzigo gani?” Alihoji Mulugo na kusisitiza kuwa hata hizo posho za siku saba zinatofautiana kati ya jiji, manispaa na halmashauri za wilaya.  Pia zinatofautiana kutokana na viwango vya elimu.
Dk Kawambwa alisema ili kuhakikisha walimu wanafundisha kwenye mazingira bora, Serikali imejipanga kujenga nyumba 264, ambazo zitakaliwa na familia mbili na ni kwa ajili ya walimu wa shule za sekondari.
Alisema awali Serikali ilipanga kuwapa walimu Sh 500,000 mara wanaporipoti, hasa wale ambao wako kwenye mazingira magumu, kwa ajili ya nyumba, lakini mpango huo umefutwa na fedha hizo zinaenda kugharimia nyumba za walimu.
“Hizi fedha anatumia zinaisha, lakini akikuta nyumba shuleni ni jambo jema kwani itamfaa yeye na wengine pia,” alisema Dk Kawambwa.

No comments: