HOMA YAPANDA VIKAO VYA CCM MJINI DODOMA...

Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi, mjini Dodoma.
Wakati Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuongoza vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) vitakavyoanza leo  mjini Dodoma, joto la nani ataingia kwenye Kamati Kuu ya chama hicho imezidi kupanda.
Kutokana na kupanda kwa joto hilo, jana baadhi ya wabunge wanaotokana na chama hicho walishuhudiwa wakiwaomba Wajumbe wa NEC wawapigie kura endapo majina yao yatajitokeza katika wale watakaotakiwa kupigiwa kura.
Hadi sasa taarifa zinasema kuwa mwenye siri ya majina ya wanaCCM watakaounda Kamati hiyo muhimu wakati ambapo chama hicho kinajiandaa na uchaguzi wa wenyeviti wa vijiji na vitongoji mwakani na pia uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ni Mwenyekiti Rais Kikwete.
Akizungumza na waandishi wa habari  mjini hapa jana, Katibu wa NEC- Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema kuwa mkutano huo utakuwa wa kawaida na utafanyika kwa muda wa siku mbili Februari 10 na 11, mwaka huu.
Alisema kuwa, pamoja na mambo mengine kikao hicho kitatanguliwa na semina ya siku mbili  kwa wajumbe wa NEC.
Alisema kuwa lengo la semina hiyo ni kuwaongezea wajumbe uelewa kuhusu masuala ya CCM na Serikali yake hasa ikizingatiwa kuwa wengi wa
wajumbe hao ni wapya kufuatia uchaguzi mkuu wa CCM uliofanyika mwaka jana.
Nape alisema kuwa, mada zitakazowasilishwa kwenye semina hiyo ni pamoja na ‘Nafasi na Wajibu wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa’, ‘Umuhimu wa Maadili kwa Viongozi na Watendaji wa CCM’,  Mikakati ya Kutekeleza Maazimio ya Mkutano Mkuu wa Taifa wa Nane wa CCM’ na Mikakati ya Kukuza Ajira Nchini’.
Alisema kuwa semina hiyo itafuatiwa na mkutano rasmi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ambao pamoja na mambo mengine utafanya uchaguzi wa Wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM.
Alisema baada ya kuundwa kwa Kamati Kuu ndipo zitaundwa kamati ndogondogo ikiwemo Kamati ya Maadili itakayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula.
Alisema kamati hiyo ndiyo itakayofanya kazi ya kushughulikia rufaa za rushwa zilizotokana na  uchaguzi mkuu wa ndani ya chama uliofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

No comments: