AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KUBAKA BINTI WA MIAKA 16...

Kijana mmoja amehukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani Mara, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kubaka binti wa umri wa miaka 16.
Aliyehukumiwa  adhabu hiyo ametambuliwa kwa jina la Amiri Bakari. Majina yake mengine ni pamoja na Njama, Ama Good na Ama Bad (18), mkazi wa Nyakato mjini Musoma.
Hukumu  hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi wa Mahakama , Janeth Msaroche, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka mahakamani hapo.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Jonas Kaijage, kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Januari 10 mwaka jana, saa 3.00 asubuhi katika eneo la Vailet Baa, mtaa wa Nyakato mjini Musoma.
Kaijage aliiambia Mahakama hiyo kuwa mshitakiwa huyo alimbaka binti huyo  aliyekuwa akipita katika eneo hilo na kwamba alimvutia katika nyumba  ambayo haijakamilika kujengwa na kisha kumbaka huku akimtishia kwa panga alilokuwa nalo kwamba iwapo akijaribu kupiga kelele angemuua.
Alisema kuwa mshitakiwa huyo baada ya kufanya unyama huo alitokomea kusikojulikana ambapo binti alikwenda kutoa taarifa kwa wazazi wake  waliokwenda katika eneo la tukio na kukuta chupi ya binti huyo na ndipo wakatoa taarifa Polisi na mshitakiwa kukamatwa.
Kabla ya hukumu hiyo kutolewa mshitakiwa alitakiwa kujitetea, ambapo aliiomba Mahakama hiyo impunguzie adhabu na baada ya hukumu kutolewa alisema kuwa  ameonewa kwani hajafanya kosa hilo na hivyo atakata rufaa.
Hakimu Msaroche alisema kuwa ametoa adhabu  hiyo kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye  tabia kama hiyo.

No comments: