WANAFUNZI 1,177 WA VYUO KUKOSA MIKOPO YA HELSB...

Jengo la Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wanafunzi 1,177 wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini, watanyimwa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB).
Hatua hiyo ilitangazwa jana baada ya wanafunzi hao kushindwa kujaza fomu za kuthibitisha mahitaji ya mikopo hiyo, kwa njia ya mtandao (OLAS). 
Kwa mujibu wa uamuzi wa HELSB uliotangazwa kupitia taarifa kwa umma katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi, hatua hiyo ni utekelezaji wa Sheria  ya Mwaka 2004 ya Bodi hiyo.
Sheria hiyo inataka wanafunzi kuomba mikopo kila mwaka. “Kwa sasa wanafunzi hao ambao orodha ya majina yao inapatikana kwenye tovuti ya Bodi www.helsb.go.tz, wamepoteza stahili yao ya kupewa mikopo.”
Bodi ilieleza kuwa iliwakumbusha waombaji wapya na wanaoendelea na masomo kuzingatia mambo muhimu ikiwamo muda wa mwisho wa kutuma maombi hayo kwa mtandao, ambao ulikuwa Agosti 31 mwaka jana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mzunguko wa kuomba mikopo hiyo kwa waombaji wote, ulifunguliwa Aprili 16 mwaka jana hadi Juni 30 mwaka huo.
Aidha, wiki moja kabla ya siku ya mwisho, Bodi kwa kupitia vyombo vya habari mbalimbali, ilitoa taarifa kuwakumbusha waombaji kuhusu tarehe ya mwisho na kuwajulisha kuwa pasingekuwa na muda wa nyongeza.
“Hata hivyo, baada ya muda huo kwisha, ilibainika wanafunzi wanaoendelea na masomo wapatao 3,702, walikuwa hawajajaza fomu na hivyo kuilazimu Bodi kuongeza muda wa wiki mbili kuanzia Julai 18 hadi 31,” ilieleza taarifa hiyo. 
Hata hivyo, licha ya kuongezwa muda huo, wanafunzi kadhaa wanaoendelea na masomo hawakuutumia kujaza fomu husika hadi ulipokwisha.
Kutokana na hali hiyo, Bodi ilimwomba Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ili waruhusiwe kuzijaza ambapo waliruhusiwa kwa masharti ya kulipa Sh 30,000 kama faini kwa kila mwanafunzi.
“Maombi hayo katika muda wa nyongeza ya mara ya pili yaliruhusiwa na mfumo wa kuyapokea kwa OLAS ulibaki wazi hadi Agosti 31, 2012. Ulipofungwa rasmi  wanafunzi wasiopungua 1,117 waliendelea kupuuza kujaza fomu hizo,” ilieleza taarifa hiyo.
Katika hatua nyingine, Bodi hiyo imerudia kutangaza kuwa utaratibu wa kuomba mikopo hiyo kila mwaka ni wa kisheria na atakayeupuuza atakuwa amejinyima stahili yake ya kupata mkopo.
Bodi hiyo imeeleza kuwa bila kufuata utaratibu huo, mwanafunzi atafikiriwa kuwa amekwisha pata kutoka katika vyanzo vingine.
Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) aliwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka Serikali ilete muswada wa kuanzisha Mfuko wa Elimu wa Wanafunzi wote wa elimu ya juu, wapate mkopo kwa asilimia 100.
Akiwasilisha hoja hiyo jana, mbunge huyo alisema hivi sasa HELSB, inakopesha wanafunzi wachache na itafika wakati itashindwa kutokana na kukosa fedha za kukopesha wanafunzi.
Alisema mfumo uliopo umekuwa unabagua wakopaji kutokana na vigezo vya kipato, uwezo na hali ya uyatima, jambo ambalo wengine wamekuwa wakitafuta vyeti vya kughushi kuonesha kwamba wamefiwa na wazazi ili wapate asilimia 100.
Mbunge huyo alibainisha vyanzo vya mapato zikiwamo hatifungani ya Serikali, tozo, riba na kampuni za simu kuchangia na vyanzo vingine ambavyo vinaweza kuchangia fedha za kutosha kutunisha mfuko wa kusaidia elimu ya juu nchini.
Alisema, Bodi katika bajeti ya mwaka 2013/14 itatumia zaidi ya Sh bilioni 500, kiwango ambacho ifikapo mwaka 2019/20 Serikali itatakiwa kutenga Sh bilioni 830 kulipia wanafunzi wachache, kitendo kinachoonesha Bodi haitaweza kulipia wanafunzi hao.
Akiwasilisha hoja ya Serikali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk  Shukuru Kawambwa alisema Serikali italeta Mswada wa Marekebisho ya Sheria,  badala ya muswada wa kuanzisha Mfuko wa Elimu ya Juu kama alivyotaka Nchemba wakati akitoa hoja binafsi.
Dk Kawambwa alisema, marekebisho hayo yatahusu Sheria ya mwaka 2001 ya Mfuko wa Elimu na Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, ili kujumuisha mapendekezo ya Nchemba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Margaret Sitta, aliunga mkono hoja, akasema Kamati yake imefanya majadiliano mara nyingi na Bodi na jambo ambalo lilikuwa halieleweki vizuri, ni vigezo vilivyotumika kupata wanufaika.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia aliunga mkono akisema marekebisho hayo yasifanywe kwa papara ili kutafuta njia bora ya kupata Mfuko, ili kuendana na maendeleo ya elimu ya juu mahali pengine duniani.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alisema mpango wa kuchangia Mfuko huo uanze na wabunge wenyewe ambao wamekuwa wakichangia harusi sasa waanze kuchangia elimu.
Bunge liliridhia hoja za wabunge na kuiagiza Serikali kuleta bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Elimu na wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alihitimisha mjadala huo baada ya wabunge kuunga mkono muswada wa marekebisho ya sheria hizo mbili. 

No comments: