SHULE 87 ZATOKA KAPA MTIHANI DARASA LA SABA...

Shule za msingi 87 za Mkoa wa Dodoma hazina mwanafunzi hata mmoja aliyefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu huku Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ikiongoza kwa kuwa na shule 37.
Haya yalibainishwa na Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Remigius Ntyama, wakati akitoa taarifa ya matokeo ya ufaulu wa wanafunzi katika Mkoa wa Dodoma.
Mbali na Kondoa kuwa na shule 37 zilizoshindwa kupeleka wanafunzi sekondari, wilaya nyingine na idadi ya shule ‘zilizofelisha’ kwenye mabano ni Chamwino (16), Mpwapwa (15), Kongwa (11), Bahi shule tano na Dodoma Mjini shule tatu.
Ntyama alisema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo, ufaulu wa wanafunzi kimkoa umekuwa ukishuka ambapo matokeo ya mwaka huu yamekuwa mabaya. Kiwango cha ufaulu kwa Mkoa ni asilimia 24.
Aidha, alisema katika baadhi ya shule kumekuwepo na tuhuma za udanganyifu kwa baadhi ya watahiniwa waliofanya mtihani huo ambapo jumla ya wanafunzi 48 walihusishwa na tuhuma hizo kutoka shule saba ambapo Bahi kuna shule mbili, Dodoma Mjini shule mbili na Kondoa shule tatu.

No comments: