MZEE MAJUTO ABAKI NJIAPANDA KIFO CHA SHARO MILIONEA...

Mwigizaji nguli nchini, Amri Athuman 'King Majuto' (kushoto) na Hussein Mkieti 'Sharo Milionea' mara baada ya kupokea moja ya tuzo zao hivi karibuni.
Wakati mwigizaji Hussein Mkieti 'Sharo Milionea’ akitarajiwa kuzikwa leo saa 10 jioni kijiji kwao,  mkongwe wa maigizo nchini, Amri Athuman ‘King Majuto’ ameeleza kushitushwa na ajali na kifo cha mwenzake huyo na kusema alikuwa mtoto pekee wa kiume katika familia yake.
Majuto anayesumbuliwa kwa kiasi fulani na kiharusi, alisema aliposikia taarifa ya msiba huo juzi usiku alishituka na kuvimba miguu na hali yake ya kiafya kuzorota kidogo, lakini hata hivyo alitumia dawa zake na kurejea kawaida.
Akizungumzia msiba huo jana, Majuto alisema umeshitua sana kwa kuwa alikuwa na malengo mengi na mwenzake na kwa sasa amebaki njiapanda kwa kuwa hajui nani wa kufanya naye kazi hizo.
Alisema walishaanza kupata kazi ya kutangaza matangazo ya Kampuni za Azam na Airtel wakiwa na    malengo zaidi ya kutafuta kampuni zingine za kufanya nazo kazi chini ya kampuni yao. 
“ Yaani mimi sijui hata nifanyeje, kwa kuwa ndio kwanza alikuwa ameanza maisha na hasa ikizingatiwa kuwa ndiye alikuwa akisaidia kwao akiwa mtoto pekee wa kiume, sasa ameiachia pengo familia yake na mimi pia. Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake,” alisema Majuto.
Sharo Milionea alizaliwa Oktoba 27, 1985 katika familia ya watoto wanne ambapo yeye alizaliwa mapacha na mwenzake (Kulwa) ambaye alifariki wakati wa utotoni. Dada zake wawili waliomtangulia kuzaliwa wako hai. Baba yao naye alishafariki miaka kadhaa iliyopita.
Katika hatua nyingine, mapema jana umati uliojumuisha baadhi ya wakazi wa wilaya ya Muheza ulifurika katika Hospitali Teule ya Wilaya hiyo kuthibitisha taarifa za kifo hicho.
Akithibitisha kifo hicho Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe alisema alikufa saa 2.30 usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Songa Maguzoni kata ya Songa wilayani Muheza katika barabara kuu ya Tanga – Segera.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo namba T 478 BVR aina ya Toyota Harrier alilokuwa akiliendesha kutoka Dar es Salaam kwenda kijiji kwao Lusanga, Muheza.
“Alipofika eneo ilipotokea ajali, gari hilo lililokuwa kwenye mwendokasi lilitoka nje ya barabara na kupinduka mara kadhaa kisha kugonga mti pembeni na kumsababishia majeraha makubwa hatimaye kifo chake papo hapo,” alisema.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa msanii huyo alikuwa akienda nyumbani kwao kusalimia wazazi  wanaoishi Lusanga akitumia gari hilo.
“Ajali hii ilitokea baada ya dereva kushindwa kumudu gari hilo kwa kuwa lilikuwa na mwendo mkali, kwa hiyo alipofika hapo liliserereka na kuacha njia na kuingia kwenye mtaro pembeni mwa njia,” alisema mkazi wa Maguzoni aliyejitambulisha kwa jina la Saidi.
Wengine walidai kuwa msanii huyo alirushwa nje ya gari baada ya ajali hiyo, kwani hata walipofika eneo la tukio walimkuta akiwa nje ya gari hilo. Walipochunguza zaidi ndani walishuhudia mifuko ya hewa imefunguka, hali inayoashiria pengine hakuwa amefunga mkanda.
Akithibitisha hilo, mtangazaji wa kituo cha redio na televisheni cha Clouds Media, Millard Ayo, aliyefika eneo hilo, alisema Sharo Milionea alikutwa nje ya gari na watu waliofika hapo mara baada ya ajali kutokea, lakini hakuwa amekata roho na hakuweza kuzungumza chochote.
“Walichungulia ndani ya gari ambalo lilikuwa limeharibika sana hawakumwona, lakini kwa pembeni nje ndiko alikuwa amelala na kwa mujibu wao, aligeuza kichwa upande wa pili na kisha kuchezesha mguu mmoja na kukata roho,” alisema Ayo.
Kwa mujibu wa wananchi wa eneo ilikotokea ajali hiyo, walishindwa kumchukua msanii huyo angalau kumkimbiza hospitalini kutokana na kijiji hicho kukosa mtu anayemiliki gari, pikipiki wala baiskeli na walipopiga simu Polisi, askari walifika hapo saa 4 usiku na kuuchukua mwili.
Diwani wa Mbaramo wilayani Muheza, Seif Makame alisema alipopata taarifa za tukio, alikwenda hospitali teule kuthibitisha, lakini hakumtambua haraka kutokana na kupasuka kichwani, ingawa baadaye alithibitisha kwa kitambulisho chake kwa msaada wa maofisa wa Polisi. Mwili wa msanii huyo unatarajiwa kuzikwa leo Lusanga.
Wasanii wengine wakubwa waliopoteza maisha mwaka huu ni Steven Kanumba, Fundi Said ‘Mzee Kipara’, Khalid Mohamed ‘Mlopelo’ na Maganga.

No comments: