IMF YASEMA UCHUMI WA TANZANIA UNAIMARIKA...

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limesema uchumi wa Tanzania umeimarika na utaendelea kuimarika siku zijazo kutokana na ugunduzi wa gesi asilia katika pwani ya nchi.
Kiongozi wa ujumbe wa IMF, Paolo Mauro alisema jana Dar es Salaam kwamba uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika ambapo Pato la Taifa kwa mwaka 2012 linatarajia kukua kati ya asilimia 6.5 hadi 7 ambapo pia mfumuko wa bei umekuwa ukipungua.
Ujumbe wa IMF ulikuwa nchini kwa takribani siku 13 kufanya majadiliano ya tathmini ya mapitio ya tano chini ya Mpango wa Ushauri wa Sera za Uchumi(PSI) na tathmini ya kwanza chini ya Mpango wa Msaada wa Dharura (SCF).
Alisema matarajio ya muda wa kati na mrefu ni kuimarika kwa uchumi hasa kutokana na ugunduzi wa gesi asilia.
Hata hivyo, Mauro aliitaka Serikali kuweka kipaumbele kuandaa mfumo wa udhibiti wa kisera kwa ajili ya kuratibu mapato yatokanayo na rasilimali ya gesi asilia utakaohusishwa na mpango wa kuandaa bajeti itakayonufaisha wananchi.
"IMF imekubaliana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha malengo ya PSI na SCF yanatekelezwa kwa kuboresha usimamiaji wa fedha za umma, tunaishauri kuandaa haraka mpango kazi wa kushughulikia changamoto katika sekta ya nishati ya umeme," alisema.
Akizungumzia utekelezaji wa programu hiyo ya PSI katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2012, Mauro alisema ni ya kuridhisha huku Serikali ya Tanzania ikifanikiwa kukusanya mapato na kudhibiti matumizi.
"Makusanyo ya mapato nchini yalikuwa mazuri na matumizi ya Serikali yalidhibitiwa ipasavyo, ingawa si madeni yote yaliyotokana na matumizi ya ndani yalikuwa yamelipwa hadi mwisho wa mwaka wa fedha.
Alisema katika utekelezaji wa mpango huo, bajeti ya mwaka 2012/13 imeweka mizani zaidi katika kuendelea kupunguza matumizi, kulinda matumizi ya huduma za kijamii na kutoa fursa kwa ajili ya kuwekeza katika miundominu muhimu.
"Mikopo ya kibiashara kutoka nje inakwenda sambamba na tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa. Programu ya PSI inalenga kupunguza msukumo wa mfumuko wa bei, kwa kudhibiti ukuaji wa fedha za msingi na ujazi wa fedha. Pamoja na mafanikio, lakini kuna ucheleweshaji wa kufikia malengo," alisema.
Kuhusu mfumuko wa bei, Mauro alisema umepungua ingawa mfumuko wa takribani asilimia 15 na usiohusisha bei za vyakula na nishati wa asilimia 9 kwa Agosti 2012 bado uko juu ya viwango vinavyotakiwa.
Alisema urari wa biashara ya bidhaa, huduma na mapato ya uchumi na uhamisho wa mali nje ya nchi una nakisi ya asilimia 16 ya Pato la Taifa, kutokana na mahitaji makubwa ya ndani, uwekezaji wa nje ambao unahusu gesi asilia na uingizaji mkubwa wa mafuta ya kuzalisha umeme baada ya uzalishaji kwa njia ya maji kupungua kutokana na ukame.
Aidha, Mauro alisema pamoja na kuwapo changamoto hususani ya upatikanaji umeme wa uhakika na wa kutosheleza mahitaji na uhakika wa kuwapo fedha za kuendeshea Shirika la UmemeTanzania (Tanesco) ukuaji wa uchumi unatarajia kuendelea kuimarika mwaka 2013.
Hata hivyo alisema deni la Tanesco kwa watoa huduma wake limeendelea kukua baada ya mpango wa dharura wa kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme kutekelezwa mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema matarajio ya muda wa kati na mrefu ni ya kuridhisha hasa kutokana na ugunduzi wa gesi asilia na kuitaka Serikali kuweka kipaumbele katika kuandaa mfumo wa udhibiti, sheria kwa ajili ya kuratibu mapato yatokanayo na rasilimali hiyo.

No comments: