MKE WA POLISI JELA KWA KUMTEKA MSICHANA...

Sakata la binti aliyetoroshwa kutoka mjini hapa akiwa darasa la saba na kupelekwa kwenye danguro mjini Mbeya, limeisha kwa mke wa askari Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) cha mjini hapa, Christina Kanoni kutupwa jela miaka 12, akihusishwa na tukio la `kutekwa’ kwa binti huyo.
Hata hivyo, pamoja na hukumu hiyo, binti huyo ambaye sasa ana umri wa miaka 14, amehuzunika akisema angekuwa hakimu, angemhukumu Kanoni kifo akidai ni binamu yake na katili sawa na muuaji.
Binti huyo mkazi wa Majengo Tanesco mjini hapa, alitoroshwa mwaka jana kwa kulishwa chakula kinachodaiwa kuwekwa dawa za kulevya na alizinduka akiwa Mbeya ndani ya danguro lenye wasichana zaidi ya 30, wote wakitumikishwa kwa biashara ya ngono.
Akizungumza baada ya hukumu ya Septemba 18 iliyotolewa na Hakimu Rosalia Mugisa wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, binti huyo alisema adhabu hiyo ni ndogo ikilinganishwa na alivyotendwa.
"Huyu hakuwa binadamu wa kawaida, ni binamu yangu lakini nadhani alistahili adhabu zaidi ya kifungo cha miaka 12," alisema huku akisikitika kuachishwa shule lakini kibaya zaidi, kuingizwa katika biashara haramu ya kutumikishwa kingono kwa takribani miezi saba, kila siku akikutanishwa na wanaume zaidi ya wawili.
Siku ya hukumu, Hakimu Mugisa alisema ameridhishwa pasipo shaka na ushahidi wa upande wa mashitaka ulioongozwa na Mwendesha Mashitaka Matiku Matiku kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo.
Akisoma hukumu, alisema: "Licha ya kutoa utetezi kuwa wewe (mshitakiwa) ni mjamzito, lakini bado nakuhukumu kwenda jela miaka 12 au kulipa faini ya Sh milioni 12 … adhabu hii kali iwe fundisho si kwako tu bali pia kwa wengine wenye tabia kama yako.
"Kitendo ulichokifanya si tu cha kinyama, lakini pia ni cha kikatili na chenye machukizo makubwa mbele ya jamii."
Wakati binti huyo akionesha kutoridhishwa na adhabu hiyo, baba yake mzazi, Michael Ndasi, babu, Edwin Ndasi (66) ambaye ni Mganga Mfawidhi katika zahanati ya Pito mjini hapa na mkewe, Lilian Ndasi (54), muuguzi wa zahanati ya Majengo waliridhika na hukumu hiyo, wakisema itakuwa fundisho kwa wengine.
Awali mwendesha mashitaka, Mkaguzi wa Polisi, Matiku, alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Februari 09, 2011 eneo la Majengo mjini hapa kwa kumrubuni msichana huyo na kumsafirisha na kumwuza Mbeya kutumikishwa kwa ngono.
Upande wa utetezi uliita mahakamani hapo mashahidi wanne akiwamo binti mwenyewe ambao walitoa ushahidi ulioiridhisha mahakama hiyo.
Binti huyo ambaye hakuhitimu elimu ya msingi baada ya kukatizwa masomo akiwa darasa la saba alikuwa tayari amesajiliwa kufanya mtihani akiwa na umri wa miaka 13, alisema tangu aingizwe katika ukahaba, hafikirii kurudia shule ya msingi, na badala yake anataka aanzie kidato cha kwanza akidai ana uwezo wa kumudu masomo.
Alisisitiza kuwa, kama akibahatika kusoma sekondari, atapenda kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanasheria ili asaidie wanyonge wanaoteseka kwa kukosa haki nchini.
Bibi wa binti huyo alikiri kuwa mjukuu wake alikuwa na uwezo mkubwa darasani na yuko tayari kumsomesha, lakini kwa masharti ya kupata shule ya bweni au hosteli yenye ulinzi mkali kwa alichosema mjukuu wake ameshaharibiwa kwani hashikiki kwa wanaume, kiasi cha wakati mwingine kutolala nyumbani.
"Nakiamini kichwa chake, lakini kisaikolojia hayuko sawa, anahitaji uangalizi wa karibu mno. Kwa sasa anapenda sana ngono, nashukuru afya yake ni njema, tumemfanyia vipimo kwa kweli hajapata maambukizi ya Ukimwi. Tunafikiria kumpeleka kwa wataalamu wa saikolojia," alisema bibi huyo.
Lakini binti akisimulia suluba alizopata katika danguro mjini Mbeya, alisema katika miezi yote saba, kuanzia siku aliyoondolewa usichana wake kwa lazima akiwa na umri wa miaka 13, hakufurahia maisha.
Alisema siku zote, yeye na wenzake walifungiwa kwa tajiri wakilindwa na walinzi watatu usiku na mchana, ingawa usiku walikuwa wakitolewa kwa kusambazwa kwenye baa na majumba ya starehe kuuza miili yao chini ya ulinzi mkali wa wapambe wa ‘tajiri’.
"Nilikuwa nalala ‘chapchap’ na wastani wa wanaume wawili usiku mmoja…matajiri wangu walikuwa wakinipeleka kwenye nyumba ya kulala wageni kwa muda, huku kila mteja akitozwa Sh 10,000 ... niliishi maisha hayo ya kuchukiza na machafu ya ukahaba kwa miezi saba hadi nilipofanikiwa kutoroka na kurudi nyumbani," alisema na kuongeza kuwa, ujira ulikuwa chakula, nguo na viatu kwa ajili ya kutokea usiku.
Aliongeza kuwa ajira hiyo isiyo rasmi mjini Mbeya ilikuwa kama sehemu ya mafunzo, kwani walioonekana kukomaa katika ukahaba, walikuwa wakisafirishwa nje ya nchi, akitoa mfano kuwa siku chache kabla ya kutoroka, wenzake 10 waliaga kuwa safari ya Urusi kwa ajili ya kazi hiyo imewadia.
Alisema alitoroka nyumba hiyo ya mateso baada ya kumwibia tajiri Sh 30,000 na kumrubuni mlinzi kisha kuondoka Julai 3 mwaka jana, bila kujua mwelekeo hadi aliposaidiwa kufika kituo cha mabasi mjini Mbeya alikopata usafiri wa kumrudisha hapa.

No comments: