ANGLIKANA WAMTAMBUA ASKOFU WA SUMBAWANGA...

Dk Dickson Chilongani.
Baada ya mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili, hatimaye maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania wameridhia Askofu Mathayo Kasagara wa Kanisa la Watakatifu Wote la Mjini Sumbawanga kuendelea kutoa huduma, huku likiwageuzia kibao waumini wanaompinga.
Waumini hao wametakiwa kurejesha mali zote za kanisa na kwamba, wakishindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Dickson Chilongani katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa.
Alizitaja mali zinazopaswa kurudishwa na kuzikabidhi kwa Dayosisi ya Ziwa Rukwa ni pamoja na Kanisa la Watakatifu wote, ofisi ya mchungaji, nyumba mbili za wachungaji, uwanja wa Kantalamba ulio na nyumba ya Askofu na Kanisa dogo la Askofu.
Mali nyingine ni jengo la ofisi ambalo halijakamilika, viwanja 14 vya kanisa vilivyopo eneo la Majumba Sita na pia shule ya msingi ya mtaala wa Kiingereza ya Mtakatifu Mathias.
"Kwa kutokabidhi mali hizo ni kukiuka maamuzi ya mahakama na Kanisa la Anglikana Tanzania halitasita kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wa kundi hilo," alisema.
Aliongeza kuwa, kikao cha maaskofu kilichokutana Septemba 26, mwaka huu mjini hapa kilitafakari kwa kina juu ya fujo zilizojitokeza katika Kanisa la Watakatifu Wote mjini Sumbawanga Septemba 23, mwaka huu zilizosababisha na kundi lisilomtambua Askofu Kasagara.
Katika vurugu hizo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa aliripotiwa kunusurika kipigo wakati wa vurugu.
Kutokana na mvutano baina ya pande mbili, upande mmoja unaoongozwa na Fulgence Rusunzu na Rojas Bendera ambao unampinga Askofu Kasagara ulifikisha mgogoro huo mahakamani, ukiomba kumzuia Kasagaraa azuiwe kutoa kuhudumu yake ya kiaskofu.
Hata hivyo, suala lao kisheria lilimalizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga, M.W. Goroba Januari 17 mwaka huu, baada ya kuzitaka pande mbili zinazovutana zimalize tofauti nje ya mahakama.
Pamoja na makubaliano hayo, chokochoko za hapa na pale hazikukoma hadi zilipotokea vurugu za hivi karibuni.
Dk Chilongani alisema kuwa, kutokana na mlolongo wa matukio, ndipo ilipoonekana kuja ulazima wa kukutana ili kulipatia ufuumbuzi tatizo la Kanisa la Watakatifu Wote la mjini Sumbawanga.
Anasema: "Kwa vile nyumba la Maaskofu wa Kanisa Anglikana Tanzania linaheshimu maamuzi ya Mahakama za Serikali, Maaskofu waliona vyema wasikilize kwanza hoja za waumini hao kabla ya kutoa uamuzi wao na hivyo kutuma tume iliyokwenda Sumbawanga baada ya vurugu za Septemba 23, mwaka huu, lakini baada ya kusikia kauli kuwa Askofu wao ni halali wakapiga kelele za kukataa kauli hiyo.
Anasisitiza kwa kusema: "Kwa mantiki hiyo, Nyumba ya Maaskofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania inatoa tamko kuwa, kulingana na Katiba ya Kanisa Anglikana Tanzania ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2004, kifungu cha 14 (8) Nyumba Ya Maaskofu imeridhika kabisa kwamba Askofu Kasagara ni Askofu halali wa Dayosisi ya Lake Rukwa."
Kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo: "Matokeo ya uchaguzi huo ni ya mwisho, hayatapingwa popote na taratibu za kumweka wakfu na kumsimika Askofu Mteule zitafuata.
Alisema kuwa nyumba ya Maaskofu inalitaka kundi hili la Wakristo wanaompinga Askofu Kasagara waelewe kwamba muumuni kuwa Mwanglikana ni suala la hiari na kama hakubaliani na mafundisho ya kanisa na maamuzi ya Maaskofu amejitenga yeye mwenyewe na kanisa na hivyo ni vyema akajitoa maana machoni mwa kanisa ni muasi na si muumini tena wa kanisa la Anglikana.

No comments: