FOLENI DAR SASA KUBAKIA HISTORIA, BARABARA ZA JUU ZAJA...

Serikali imetangaza mkakati wa kupunguza foleni Dar es Salaam ikiwamo kuanza ujenzi wa maegesho ya vivuko na boti kati ya Jiji hilo na Bagamoyo na ujenzi wa barabara ya juu kuanzia eneo la Tazara.
Sambamba na hilo, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli amewashambulia baadhi ya wabunge kuwa wanapitisha sheria ya kubomoa nyumba za kwenye hifadhi ya barabara na wanashiriki kutetea wananchi wasibomolewe nyumba kwenye hifadhi hizo.
Akiwasilisha jana makadirio ya matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2012/13 akiomba Bunge kuidhinisha Sh trilioni 1.02 na kati ya hizo, Sh bilioni 300.7 ni kwa ajili ya Mfuko wa Barabara utakaojenga na kufanyia matengenezo barabara kadhaa nchini.
Katika kukabiliana na msongamano Dar es Salaam, Magufuli alibainisha mipango itakayotekelezwa mwaka huu wa fedha kuwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za pete, barabara ya juu katika eneo la Tazara, ujenzi wa maegesho ya vivuko na boti kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo na ujenzi wa barabara za lami ikiwamo kuzifanyia upanuzi.
Dk Magufuli alisema mwaka huu wa fedha miradi hiyo ya Dar es Salaam imetengewa Sh bilioni 899.06 ambapo kwa upande wa ujenzi wa maegesho ya vivuko na boti kutakuwa vituo kwa watakaotumia usafiri huo.
"Mradi huu utatekelezwa hatua kwa hatua ambapo Sh bilioni 3.5 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa maegesho mwaka huu," alisema.
Kuhusu barabara ya juu eneo la Tazara na barabara za maingiliano, alisema ujenzi utaanza mwaka huu na tayari upembuzi yakinifu na usanifu umeshafanyika kwa ufadhili wa Shirika la Misaada ya Kimataifa la Japan (JICA).
Gharama za ujenzi zinatarajiwa kuwa Sh bilioni 60 lakini mwaka huu wa fedha zimetengwa Sh bilioni mbili ambazo ni za ndani.
Alisema barabara za pete zenye urefu wa kilometa 98.15 zitajengwa na fedha zilizotengwa ni Sh bilioni 10.577 kwa ajili ya ujenzi, kufanya upanuzi na kukarabati barabara hizo.
Waziri alisema barabara zilizokasimiwa Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (Tanroads) zenye urefu wa kilometa 78.64 zimetengewa Sh bilioni 4.398  matengenezo yao.

No comments: