APANDISHWA KIZIMBANI KWA KUKASHIFU ASKARI WA UINGEREZA WALIOKUFA KWA BOMU...

Kijana mmoja juzi amefikishwa mahakamani kwa kutuma meseji za uchokozi kwenye mtandao wa Facebook kuhusu vifo vya askari sita wa Uingereza.
Azhar Ahmed mwenye miaka 19 amedaiwa kutenda kosa hilo chini ya Sheria ya Mawasiliano ya kutuma meseji za kichokozi.
Hapo kabla alionekana hana hatia katika mashitaka hayo na alitarajiwa kufikishwa mahakama ya Hakimu Mkazi ya Huddersfield jana.
Ahmed anadaiwa kutuma meseji za matusi kwenye Facebook katika ukurasa wake Machi 8, mwaka huu ikiwa ni siku mbili tu baada ya askari hao wa Uingereza kuuawa kwenye mlipuko nchini Afghanistan.
Ahmed aliingia mahakamani hapo akiwa kavalia kofia na fulana nzito nyeupe inayofunika kichwani ya mikono mirefu.
Jaji wa Mahakama ya Wilaya alielezwa ushahidi haujakamilika na kuahirisha hukumu hadi Septemba 14, mwaka huu kufuatia matatizo ya kisheria ambayo hayakutarajiwa.
Ahmed anayeishi Ravensthorpe huko West Yorkshire, aliachiwa kwa dhamana.
Kati ya waandamanaji 20 na 30 wa mrengo wa kulia walihudhuria mahakama ya Huddersfield kusikiliza na kujaza sehemu yote wanayokaa wananchi mahakamani hapo.
Katika hatua za mwanzo waandamanaji wapatao 50 walifanya maandamano ya kelele wakishinikiza wale wote wanaokashifu vikosi vya Uingereza kufungwa jela.
Maoni katika Facebook Machi mwaka huu yalimiminika kufuatia vifo vya askari hao sita wa Uingereza. Askari sita waliuawa kwenye tukio moja baya zaidi kutokea kwa vikosi vya Uingereza nchini Afghanistan tangu mwaka 2001.
Askari waliokufa, watano kati ya hao walikuwa kati ya umri wa miaka 19 na 21. Waliuawa wakati gari lao walilokuwa wakitumia kulipuliwa na kitu chenye nguvu kubwa.

No comments: