Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad amejiuzulu wadhifa wake jana kutokana na kuzama kwa meli ya mv Skagit.
Taarifa ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,Dk. Abdulhamid
Yahya Mzee ilisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohammed Shein amekubali ombi la Waziri Masoud kujiuzulu.
“Tarehe 20 Julai, 2012 Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Mheshimiwa Hamad Masoud
Hamad alimwandikia barua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohammed Shein ya kumuomba ajiuzulu kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya mv. Skagit iliyotokea Julai 18, 2012,” ilisema sehemu ya taarifa ya Dk Mzee.
Kufuatia kujiuzulu kwa waziri huyo, Rais Dk Shein amemteua Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF), Rashid Seif Suleiman kuwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano.
Uteuzi wa Waziri mpya wa Miundombinu na Mawasiliano umeanza jana .
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk Shein ameunda Tume ya kuchunguza ajali ya kuzama kwa meli ya mv. Skagit.
Mwenyekiti wa Tume hiyo ni Jaji Abdulhakim Ameir Issa. Wajumbe ni Meja Jenerali S. Omar, Hassan Mussa Mzee, Kapteni Abdulla Yussuf Jumbe, Kaptein Abdulla Juma Abdulla, Salum Taoufiq, Kaptein Hatibu Katandula, Mkali Fauster Ngowo, Ali Omar Chengo na Shaaban Ramadhan Abdalla ambaye ni Katibu wa Tume.
No comments:
Post a Comment